Watu takriban 70 wamekufa na wengine kadhaa wakihofiwa kufunikwa na kifusi baada ya jengo lenye ghorofa nane kubomoka nchini Bangladesh katika mji mkuu wa Dhaka.
Juhudi zinaendelea kufanyika ili kuwaokoa watu waliofunikwa na kifusi cha jengo hilo ambapo watu wasiopungua 200 wamejeruhiwa.
Sasa imekuwa sio ajabu kwa matukio ya majengo kubomoka nchini Bangladesh kutokana na maghorofa mengi kujengwa bila kufuata taratibu sahihi za ujenzi.
Jengo hilo lililokuwa na ghorofa nane lilikuwa na maduka makubwa, kiwanda cha nguo, benki na maduka mengine kadhaa ya kawaida.
Watu wengi wamekusanyika nje ya jengo hilo wakitaka kujua hatma ya ndugu, marafiki na jamaa zao kufuatia jengo hilo kubomoka wakati ambapo kila mtu alikuwa ‘bize’ kwa shughuli zake.