Hospitali ya Grenoble na meneja wa Michael Schumacher Sabaine Kehm wamethibitisha kuwa bingwa wa dunia mara 7 katika mashindano ya Formula 1, Schumacher ametoka katika hali ya mahututi, hali aliyokaa nayo kwa miezi sita na ametoka hospitali na amewasiliana na mke wake na watoto.
Michael Schumacher alikuwa akitibiwa majeraha mabaya katika sehemu ya kichwa kutokana na ajali mbaya iliyotokea Desemba 29 Alpes Ufaransa katika michezo ya kuteleza kwenye barafu na kupelekea hadi kuwa mahututi.
“Michael ametoka CHU Grenoble lakini atakuwa akiendelea na matibabu na hayupo maututi tena” alisema Sabine Kehm. “Familia yake inapenda kushukuru madaktari wote, wauguzi na wengine wote katika hospitali ya Grenoble na wale waliomsaidia pale katika eneo la ajali na wale waliofanya kazi nzuri katika ile miezi ya mwanzo” aliongeza Sabine.
Kufuatia kutoka Michael Schumacher katika hospitali ya Grenoble, itaongezwa muendelezo wa matibabu, atakuwa akitibiwa katika hospitali ya Lausanne, huko magharibi mwa Switzerlandkwa sasa.
“Familia pia imeendelea kutoa shukrani kwa watu wote ambao walimtumia Michael meseji za kumtakia mema tuna uhakika zilisaidia, na kwa siku zijazo tunaomba watu waelewe kwamba matibabu yake kwa sasa haitajulikana ni wapi anapopatiwa matibabu” alisema Kehm.