Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdul habib Fereji
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema suala la kupima Ukimwi ni la hiari kwa hivyo hakuna mwananchi wala mgeni atakayelazimishwa kufanya hivyo endapo akitaka kufunga ndoa au akipatiwa ajira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdul habib Fereji aliwaambia wajumbe wa baraza la wawakilishi jana wakati akijibu swali la nyongeza la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe ( CUF) Salim Abdalla Hamad aliyetaka kujuwa kwa nini Serikali isipime afya za wananchi kwa lazima kujuwa kama wapo salama na ugonjwa wa Ukimwi.
Fereji alisema Zazibar hakuna sheria inayoilazimisha Serikali kuwapima wananchi afya zao kwa lazima kuhusu ugonjwa wa Ukimwi na kwa kuwa hilo ni suali la mtu binafsi serikali yake ni kutoa elimu na kuwahamasisha wapime afya zao lakini sio kuwalazimisha.
Waziri huyo alisema hali hiyo inatokana na Azimio la dunia ambapo linakataza kufanya hivyo ni kwenda kinyume na haki za Binaadamu wakati Tanzania imesaini mkataba wa kimataifa wa kuheshimu haki za binaadamu.
“Naibu Spika azimio la dunia linatukataza kupima wananchi afya zao kwa lazima kujuwa kama wapo salama na ugonjwa wa Ukimwi kwa hivyo Tanzania tumesaini mkataba wa azimio hilo hatuwezi kwenda kinyume na hatuwezi kufanya hivyo kwani tutakuwa tukienda kinyume na maazimio ya kimataifa” aliongeza.