Jeshi la polisi nchini Tanzania limekipiga marufuku chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA)kufanya shughuli zozote za kuaga miili ya marehemu kwenye viwanja vya Soweto kwani zoezi la uchunguzi bado linaendelea kwenye viwanja hivyo huku mabomu yakirindima uwanjani hapo.
Akizungumza ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoani Arusha Liberatus Sabas amesema kutokana na uchunguzi unaoendelea wa tukio la bomu kwenye viwanja hivyo, imeona kuwa si busara kuweka mkusanyiko wa watu kwani kutaharibu upelelezi.
Kamanda Sabas ameema jeshi hilo limewataka viongozi wa chama hicho kuwaeleza wafuasi wao mahali sahihi watakapoweza kufanyia shughuli hiyo lakini si kwenye viwanja hivyo.
Hali kwenye viwanja hivyo imekuwa ya pilika pilika tangu juzi kwa wafuasi wa chama hicho kujikusanya tokea asubuhi hadi jioni kwa madai ya kuomboleza tukio la bomu la kurushwa kwa mkono lililotokea uwanjani hapo.
Hata hivyo viongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo walikuwa wamekusanyika kwenye uwanja huo hali iliyoendelea kuleta mvutano kati ya viongozi wa jeshi la polisi na wafuasi hao, baada ya kukaidi amri ya jeshi hilo, kitendo kilichopelekea mabomu ya machozi kuribndima uwanjani hapo.
Baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho waliokuwepo uwanjani hapo akiwemo mbunge wa jimbo la Ubungo Mh. John Mnyika, Ezekia Wenje, huku wabunge mbali mbali wa chama hicho wakiwa kwenye kikao cha bunge kinachoendelea.