
Kulingana na maelezo ya shirika la afya duniani mama mwenye virusi vya ukimwi kwa nchi zilizo endelea na zenye upatikanaji mzuri wa maji safi na salama anashauriwa kutomnyonyesha mtoto ili kumkinga na uwezekano wa kumuambukiza virusi vya ukimwi.
Huku kwa nchi maskini na zisizo na upatikanaji mzuri wa maji safi na salama wanashauriwa kuwanyonyesha watoto wao huku wakiendelea kupatiwa matibabu ya kufubaza virusi hivyo, ningependa kufahamu kwa hapa kwetu Tanzania ni tahadhari gani/ushauri gani kina mama hao hupewa ili kuwakinga watoto wao?
Naamini humu kuna madaktari na/au waliokwisha pewa ushauri unaohusiana na jambo hili, tafadhali tushirikishane
Mambo yanayochangia kuongeza hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
• Mama kuambukizwa virusi vya UKIMWI wakati wa ujauzito au wakati wa kunyonyesha:
Nyakati hizi mama ana virusi vya UKIMWI vingi kwenye damu na hivyo uwezekano wa kumwambukiza mtoto ni mkubwa;
• Mama kuwa na UKIMWI: Uwezekano wa kumwambukiza mtoto ni mkubwa kwani mama atakuwa na virusi vya UKIMWI vingi mwilini mwake;
• Mama kuwa na maambukizi ya magonjwa ya ngono wakati wa ujauzito:
Magonjwa ya ngono husababisha vidonda vidogo ukeni ambayo huongeza hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI;
• Taratibu zinazotumika wakati mama anapojifungua: Kwa mfano kuongeza njia ya uzazi, uchanaji mapema wa utandu, kumnyonya mtoto uchafu baada ya kuzaliwa n.k;
• Hali ya lishe ya mama: Mama mwenye hali nzuri ya lishe ana mfumo thabiti wa kinga na hivyo kuchelewesha mama huyo kupata UKIMWI;
• Hali ya matiti ya mama: Matiti yenye vidonda au michubuko, chuchu zinazotoa damu na majipu ya titi huongeza hatari ya mama kumwambukiza mtoto wake iwapo mtoto atanyonyeshwa;
• Muda wa kunyonyesha: Hatari ya uambukizo huongezeka iwapo mama mwenye virusi vya UKIMWI atamnyonyesha mtoto wake kwa zaidi ya miezi sita;
• Kuchanganya maziwa ya mama na vinywaji au vyakula vingine:
Kuchanganya maziwa ya mama na vinywaji kama maziwa mbadala, maji, chai, uji, maji ya matunda n.k. huweza kusababisha mikwaruzo kwenye utumbo wa mtoto na hivyo kutoa mwanya kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI;
• Hali ya kinywa cha mtoto: Vidonda vya kinywani au kooni na utandu mweupe kinywani kwa mtoto huweza kuongeza hatari ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia sehemu hizo zenye vidonda.
Ikumbukwe kuwa njia kuu ya kuzuia mtoto kupata virusi vya UKIMWI ni wazazi kuzuia
wasiambukizwe virusi hivyo. Jukumu hili ni la baba na mama.
