Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Mbunge wa jimbo la Hai, Mhe. Freeman Mbowe leo Jumatatu 8/8/2016 ameongoza viongozi wa vyama vya siasa na Serikali na wananchi kuchangia umaliziaji wa ujenzi wa hospitali ya Sambarai iliyopo Kibosho mkoani Kilimanjaro.
Bibi Gaudensia Stambuli Kilawila ambaye amefariki na umri wa miaka 94 ni mama mzazi wa Mwenyekiti wa halmshauri ya Moshi vijijini, Mhe. Michael Kilawila, kabla hajafariki alimwambia mtoto wake huyo kwanini isijengwe hospitali ambayo wazee watatibiwa hapo haitawalazimu kwenda mbali kupata matibabu kama ilivyokuwa kwake.
Hospitali ya Sambarai iliyopo Kibosho, Moshi vijijini inahitaji Shilingi milioni 17 kumalizia ujenzi wa hospitali wake ikiwemo na kuwekewa umeme, ambapo Mhe. Mbowe amechangia katika kukamilisha kuwekwa umeme kwa kuchangia Shilingi Milioni 2.5.
Hospitali hii itakuwa ni kumbukumbu njema kwa mama Gaudensia, viongozi wengine waliochangia ni pamoja na Mameya wa halmsahauri, wenyeviti,madiwani na wananchi waliohudhuria msiba huo.
Akiongea kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Chama na wabunge, Mhe. Mbowe ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wengine wote ambao msiba huo umewagusa.
Pia ametoa shilingi milioni 1 kama mchango kwa niaba ya Mbunge wa Moshi vijijini, Mhe. Anthony Kombu ambaye amempa majukumu muhimu kuyafanya nje ya Kilimanjaro ndo maana hakuweza kuhudhuria msiba huo wa mama wa Mwenyekiti wake wa halmashauri ya Moshi vijijini Mhe. Kilawila.
Aidha akiendelea kuongea mbele ya waombolezaji Mhe. Mbowe amesema linapokuja suala la kushirikiana na jamii haina budi kuweka tofauti za kisiasa pembeni na kushirikiana na jamii nzima, pia siku aliyozaliwa bibi Gaudensia ndiyo siku aliyozaliwa baba yake Mbowe, Mbowe amewataka waombolezaji wasisikitike sana kwa kuondokewa na mpendwa wao, bali washukuru kwa yote, kwani kifo ni njia ya kila mmoja.
“Tusisikitike sana, kifo ndiyo njia ya kila mmoja wetu, kama alivyosema Paroko, kila mtu atengeneze njia yake, tupendane ndio Mungu hupenda nae alituagiza upendo, bibi Gaudensia ni mfano, hata kwa jinsi watu walivyojaa ni ishara alikuwa akishirikiana na kupendana na jamii inayomzunguka ” amesema Mbowe.
“Mtu mwema, aliyependana na.watu na kushirikiana nao anapofariki watu huhuzunika lakini hakuna haja ya kuhuzunika leo yeye, kesho hatujui ni zamu ya nani, hivyo tuyaandae maisha yetu kwa kufanya yale yanampendeza Mungu na jamii, katika nyumba za ibada makinisani na misikitini tunafundishwa kutenda yaliyo mema.mbele za Mungu siku zote, nakupa pole sana Mhe. Kilawila, ndugu,jamaa na marafiki kwa mara nyingine kwa msiba huu mzito wa bibi yetu Gaudensia, Bwana alitoa, Bwana ametoa jina lake lihimidiwe” ameongeza Mbowe.