Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete Jana Jumatatu, Aprili 15, 2013, ameanza ziara rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika Ufalme wa Uholanzi kwa mwaliko wa Her Majesty Malkia Beatrix wa nchi hiyo.
Rais Kikwete akiambatana na Mama Salma Kikwete na ujumbe wake ameondoka nchini mchana wa jana, Jumapili, Aprili 14, kwenda Uholanzi tayari kwa ziara hiyo ambako pia ataandamana na Mawaziri wanne wa Serikali.
Mawaziri hao ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Bernard Membe, Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dr. Abdallah Kigoda, Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Maji, Ardhi, Nishati na Maendeleo ya Makazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Ramadhan Shaaban.
Katika siku ya kwanza ya ziara yake jana, Rais Kikwete alifanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya Tanzania na Uholanzi kwenye Makazi Rasmi ya Waziri Mkuu.
Mazungumzo hayo rasmi yalkkuwa kati ya Rais Kikwete na ujumbe wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uholanzi Mheshimiwa Frans Timmermans.
Baada ya mazungumzo hayo rasmi, Rais Kikwete alikutana kwa mazungumzo na HRH Princes Maxima, Mke wa Mfalme Mtarajiwa wa Uholanzi, Prince of Orange Willem Alexander ambaye anatarajiwa kurithi kiti cha Ufalme kutoka kwa Mama yake, Malkia Beatrix, mwishoni mwa mwezi huu, Aprili 30, 2013.
Baadaye, Rais Kikwete na ujumbe wake atakutana na kufanya mazungumzo na Her Majesty Malkia Beatrix wa nchi hiyo ambaye anastaafu rasmi Aprili 30 mwaka huu kumwachia nafasi hiyo mwanawe, Prince Willem Alexander.
Miongoni mwa shughuli zake nyingine jana Rais Kikwete alikutana na uongozi wa Kampuni ya Rijk Zwaan Netherlands Limited, atakula chakula cha mchana cha kazi na wawakilishi wa Jumuiya ya Biashara ya Uholanzi na baadaye atakutana kwa mazungumzo na viongozi wa Chama cha Wenye Viwanda na waajiri wa nchi hiyo.
Leo, Jumanne, Rais Kikwete atatembelea Bandari ya Rotterdam, moja ya bandari maarufu zaidi duniani, atakutana kwa mazungumzo ya faragha kati yake na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mheshimiwa Mark Rutte ambaye pia watakula naye chakula cha mchana.
Mchana, Rais Kikwete atatembelea Kampuni maarufu ya mafuta duniani ya Shell na kukutana na jumuiya ya Watanzania wanaoishi Uholanzi.
Rais Kikwete na ujumbe wake anatarajiwa kurejea nchini Jumatano, Aprili 17, 2013.
Imetolewa na:Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,Ikulu.
Dar es Salaam.
15 Aprili, 2013