Viongozi wa vyama vya upinzani vya CHADEMA, NCCR MAGEUZI na CUF wamesisitiza madai yao ya kutaka kurejeshwa bungeni muswada wa marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, ili kuendelea na mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya yenye ridhaa ya watanzania wote.
Wakizungumza katika mahojiano maalum na CHANNEL TEN mara baada ya kushiriki kipindi cha majadiliano cha BARAGUMU leo asubuhi viongozi hao FREEMAN MBOWE wa CHADEMA, JAMES MBATIA wa NCCR MAGEUZI na Profesa IBRAHIM LIPUMBA wa CUF wamesema kilichofanyika bungeni kwa wabunge wa CCM kupitisha muswada huo wa sheria ya mabadiliko ya katiba kibabe kutaliweka taifa hili katika wakati mgumu kupata katiba bora yenye maslahi kwa watanzania wote
Wapinzani walisusia mjadala wa sheria ya mabadiliko ya katiba bungeni hivi karibuni wakiwa na madai kadhaa kubwa ni kutoshirikishwa wananchi wa upande wa Zanzibar, vipengele vya muswada huo vinavyompa madaraka makubwa Rais wakati wa upatikanaji wa wajumbe wa bunge maalum la katiba na pia kipengele kinachoivunja tume ya mabadiliko ya katiba mara tu tume hiyo inapokabidhi rasimu kwenye bunge la katiba.
Credit: Baragumu Channel Ten