Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imezipiga marufuku kampuni zote zinazojishughulisha ukamataji na ufungaji magari yaliyoegeshwa kiholela kutokana na malalamiko mbali mbali ya wananchi ambayo ni pamoja na kufungiwa na kuharibiwa magari,rushwa pamoja na kampuni hizo kufanya kazi kinyemelea kinyume cha sheria.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick katika kikao cha kamati ya Ushauri ya mkoa, (RCC) kinachojumuisha wakuu wa wilaya, wabunge, wakurugenzi wa manispaa pamoja watendaji wa jiji la Dar es Salaam.
Aidha mkuu wa mkoa ameagiza kuchukulia hatua za mara moja katika kuhakikisha jiji linakuwa safi kwa kushughulikia kero ya uchafu, upangaji ovyo wa bidhaa kando za barabara hasa maeneo ya katikati ya jiji, pamoja na tatizo la ombaomba ambalo limeonyesha kushamiri kila kukicha.