Zaidi ya wasichana milioni 30 wako katika hatari ya kukeketwa katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Hii ni kwa mujibu wa shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto la Unicef.
Shirika hilo limesema kuwa zaidi ya wasichana milioni 125 na wanawake walio hai hii leo wamefanyiwa ukeketaji, kitendo ambacho leo kinapingwa na nchi nyingi ambako vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika.
Kitendo cha kukata sehemu za siri za wasichana kinafanywa sana katika baadhi ya nchi za kiafrika , Mashariki ya kati na miongoni mwa jamii za Bara Asia ikiaminiwa kulinda ubikira wa wanawake.
Shirika la Unicef linataka hatua kuchukuliwa ili kukomesha kitencho hicho.
Utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa, ambao unasemekana kuwa wa hivi karibuni kabisa kuhusu swala hilo, uligundua kuwa juhudi za kupinga ukeketaji zimeshuka sana miongoni mwa wanaume na wanawake.
Kitendo cha ukeketaji au tohara kwa wasichana, ni ukiukwaji mkubwa wa haki ya kiafya ya msichana, uzima wake na bidii yake,” alisema naibu afisaa mkuu mtendaji wa shirika la Unicef Geeta Rao Gupta,
“kinachobainika wazi kwenye ripoti hii ni kuwa sheria pekee haitoshi.”
Ripoti hiyo yenye mada ”Upashaji tohara wa wasichana: takwimu na uchunguzi wa mambo yanavyobadilika” ilitolewa rasmi mjini Washington DC.
Utafiti huo uliokusanywa kutokana na data ya zaidi ya miaka 20 iliyopita kutoka katika nchi 29, barani Afrika na Mashariki ya Kati ambako ukeketeaji ungali unafanywa, uligundua kuwa wasichana wako katika hatari ndogo ya kukeketwa kuliko ilivyokuwa miaka 30 iliyopita.
Sasa hivi nchini Tanzania na Kenya, wasichana hawako katika hatari ya kukeketwa kama walivyokuwa akina mama zao huku viwango vya ukeketaji vikipungua maradufu nchini Benin, Jamuhuri ya Afrika ya Kati, nchini Iraq, Liberia and Nigeria.
Lakini ukeketaji unasalia kuwa kitendo kikubwa sana nchini Somalia, Guinea, Djibouti na Misri na pia vimepungua nchini Chad, Gambia, Mali, Senegal, Sudan na Yemen.
Hata hivyo, haikuona ushahidi wowote wa wasichana, wanawane , wanaume na vijana kupinga kitenco hicho.
Nchini Chad, Guinea na Sierra Leone wanaume zaidi kuliko wanawake walitaka sana kuona kitendo hicho kikikomeshwa.
“changamoto sasa ni kuhamasisha wanawake na wasichana kuanza kupinga kitendo hicho , wanaume na vijana wanakipinga huku wakikata kitendo hicho wanachosema ni udhalilishaji kukomeshwa,” alisema Bi Rao Gupta.
Ripoti hiyo inapendekeza umma kuwezeshwa kuzungumzia zaidi swala hilo ili tamaduni za kijamii ambazo zinakiuka kitendo hicho kulaaniwa vikali.
Katika baadhi ya jamii ukeketeji, ni utamaduni ambao unahakikisha kuwa wasichana wanasalia kuwa bikra hadi kuolewa.