Willy Mutunga rais wa mahakama ya juu zaidi Kenya.
Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya, imeamua kuwa rais mteule Uhuru Kenyatta atasalia kuwa rais mpya wa Kenya baada ya kusema kuwa uchaguzi ulifanywa kwa njia huru na ya haki.
Uchaguzi wenyewe ulifanyika tarehe nne mwezi Machi, ambapo hesabu ya kura ilimpa ushindi Kenyatta kwa zaidi ya laki nane.
Rais wa mahakama hiyo jaji mkuu Willy Mutunga alisema kuwa mahakama imekubali kwa kauli moja kuwa uchaguzi ulifanywa kwa njia ya huru na wazi na kuwa Kenyatta na mgombea mwenza wake walichaguliwa kihalali.
Uamuzi huu una maana kuwa Uhuru Kenyatta ndiye ataapishwa kama rais mpya wa Kenya tarehe tisa mwezi ujao
Kesi hiyo iliwasilishwa katika mahakama ya juu zaidi na mpinzani mkuu wa Kenyatta, Raila Odinga baada ya uchaguzi uliofanyika mapema mwezi huu.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa Uhuru alishinda uchaguzi kwa kumpiku Raila kwa asilimia 50.07 huku Raila akipata asilimia 43.28. Matokeo haya yalizuia kufanyika kwa duuru ya pili ya uchaguzi kwa kura 8,100.Bwana Odinga aliishutumu tume huru ya uchaguzi na mipaka kwa kuhujumu matokeo ya uchaguzi ili kumpa ushindi Uhuru Kenyatta.
Uchaguzi wa urais, wabunge na wajumbe wengine wa serikali, ulifanyika tarehe nne mwezi Machi, ukiwa wa kwanza tangu uchaguzi uliokumbwa na ghasia mwaka 2007 na kusababisha vifo vya watu zaidi ya elfu moja.
1 Comment
frankly kenyata is deserved to be a president of kenya