Kasi ya kukamatwa kwa Watanzania wakiwa wamebeba dawa za kulevya nje ya nchi, imezidi kuchukua sura mpya baada ya kubainika kuwa maelfu ya Watanzania wanatumikia vifungo mbalimbali ikiwamo vifungo vya maisha nje ya nchi.
China pekee mpaka sasa ina Watanzania 176 wanaotumikia vifungo katika magereza za nchi hiyo, huku asilimia 99 wakiwa wamekamatwa na dawa za kulevya.
Kutokana na kuwapo ongezeko hilo la wafungwa wa dawa za kulevya, China imekataa ombi la Tanzania la kubadilishana wafungwa, ikieleza hatua hiyo itachochea watu wengine kujiingiza kwenye uuzaji wa dawa za kulevya nchini humo.
Hatua hiyo imekuja baada ya nchi hizo mbili kutofautiana katika mfumo wa sheria, ambapo China mtu anayekamatwana dawa hizo hunyongwa hadi kufa wakati Tanzania mtu anayekutwa na dawa hizo anahukumiwa kifungo.
Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema: “Takwimu halisi tulizonazo kutoka China pekee zinaeleza kuwa Watanzania 176 wanatumikia vifungo na asilimia 99 ni kwa tuhuma za dawa za kulevya.
Kawaida nchi hiyo adhabu yake ni kifo lakini kesi nyingi bado zipo katika uchunguzi ambao huchukua miaka miwili.”Hata hivyo alisema kutokana na uhusiano mzuri wa nchi hizi mbili, kuna uwezekano mkubwa kwa Watanzania hao kufungwa kifungo cha maisha pamoja na faini.
Aidha, alisema juhudi za Tanzania kuwasiliana na China kuhusu uwezekano wa kuwa na mikataba ya kubadilishana wafungwa ziligonga mwamba, baada ya nchi hiyo kukataa ombi hilo kutokana na idadi kubwa ya wafungwa hao kutuhumiwa na dawa za kulevya.“China imekataa kuwa na mkataba wa kubadilishana wafungwa kwani wanahofu kuwa inaweza ikachochea biashara hivyo.
Hivyo kinachofanyika ni kuwatembelea wafungwa hao mara kwa mara na kuhakikisha wanapata haki zao na kuwasaidia mawasiliano wao na ndugu zao wanapotumikia vifungo vyao nchini humo.”Wakati hayo yakibainika, Jumanne wiki hii Tanzania ilisaini mkataba wa kubadilishana wafungwa na Thailand, mkataba ambao utawafanya Watanzania waliofungwa nchini humo kuomba kutumikia vifungo vyao nchini.
Hata hivyo, takwimu zilizotolewa na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, zinaeleza kuwa zaidi ya Watanzania 103 wamekamatwa nchini Brazil kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya, huku 132 wakikamatwa katika nchi nyinginezo.
Hata hivyo, taarifa zaidi kutoka katika tume hiyo zinadai kuwa hiyo si takwimu halisi ya Watanzania wanaoshikiliwa nje ya nchi, bali imetokana na nchi hizo kutoa taarifa kuhusu Watanzania hao, kwani bado idadi kubwa ya Watanzania wanakamatwa lakini taarifa zao hazijaweza kuifikia tume.Akizungumza na Mwananchi Jumamosi jana Kamanda wa Polisi Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema tatizo la dawa za kulevya linazidi kuwa kubwa kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya wasafirishaji na watumiaji hapa nchini.
Chanzo:Mwananchi