WANAFUNZI zaidi ya ishirini wenye umri wa kati ya miaka 7 – 9 wa shule ya kimataifa ya St Charles iliyopo Don Bosco katika Manispaa ya Iringa wamenusurika kifo baada ya gari waliyokuwa wamepanga lenye namba T415AEG kushindwa kupanda mlima na kupinduka.
Ajali hiyo imetokea jana mchana katika eneo la Msikiti wa Hidaya katika kata ya Mvinjeni katikati ya mji wa Iringa.
Walioshuhudia tukio hilo wamesema daladala hilo lilikuwa likitokea eneo la FRELIMO katika Manispaa ya Iringa kuelekea mjini Iringa na baada ya kufika eneo hilo lilishindwa kupanda mlima na kuanza kurudi nyuma kwa kasi kabla ya kupinduka.
Alisema shuhuda, Juma Omari kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva ambaye alionekana kuendesha gari hilo kwa bila kuchukua tahadhari pamoja na kutambua kuwa mbele kuna kona na mlima.
Anasema, wananchi walitoa msaada wa kuwatoa katika daladala na kuwakimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Katika ajali hiyo hakuna aliyepoteza maisha zaidi ya mwanamke mmoja ambae jina lake bado kufahamika aliyejeruhiwa vibaya mikono yake.
Mmoja kati ya wauguzi wa Hospitali ya mkoa wa Iringa ambae hakutaka kutaja jina lake kwa kuwa si msemaji wa Hospitali hiyo alisema kuwa hali za watoto hao si mbaya sana zaidi ya kupata michubuko midogo midogo.