Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Erasmus Mrosso maarufu kama Mnyee (35), kulipa faini ya Sh. 700,000 au kwenda jela miaka miwili baada ya kupatina na hatia ya kosa la kukutwa na bastola isivyo halali.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi, Thomas Simba, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka kuthibitisha makosa bila kuacha shaka.
Hakimu Simba alisema ushahidi wa mashahidi watano wa Jamhuri uliotolewa mahakamani hapo ulieleza kwamba askari polisi walipofanya upekuzi nyumbani kwa mshtakiwa walikuta bastola, lakini hawakuona kibali cha umiliki wake.
Alisema mshtakiwa alipopata nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma hizo, hakuileza mahakama kama alikuwa na kibali cha kumiliki bastola hiyo au la.
“Mshtakiwa ameshindwa kuieleza mahakama kuhusu umiliki wa bastola hiyo na imemtia hatiani kwa kosa la kukutwa na silaha kinyume cha sheria,” alisema Hakimu Simba.
Alipopewa nafasi ya kujitetea ili apunguziwe adhabu, mshtakiwa alidai kuwa amekaa mahabusu muda mrefu mahakama impunguzie adhabu.
Hakimu alisema mshtakiwa atalipa faini hiyo na akishindwa atatumikia kifungo cha miaka miwili jela.
Hadi NIPASHE inaondoka mahakamani hapo mshtakiwa alishindwa kulipa faini na alikwenda jela kutumikia kifungo hicho.
Katika kesi ya msingi, mshtakiwa anadaiwa kuwa Agosti 3, mwaka 2011 eneo la Magomeni Kagera, Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alikutwa na bastola bila kibali.
CHANZO: NIPASHE