Miaka miwili iliyopita msanii maarufu wa kike duniani Angelina Jolie ambaye pia ni mke wa msanii mkubwa Brad Pitt alitangaza kufanyiwa upasuaji wa kukata matiti yake yote mawili kama njia ya kujiepusha na hatari ya kupata kansa ya matiti.
Hivi karibuni Angelina Jolie ametangaza kufanyiwa upasuaji mwingine mkubwa wa kuondoa mirija yake ya uzazi pamoja na kizazi chake, Angelina amelazimika kuchukua uamuzi huo ikiwa ni hatua za lazima ili kujiepusha na saratani ya kizazi.
“Haikuwa rahisi kufanya maamuzi haya ya kuondoa kizazi” Angelina Jolie aliandika kwenye makala iliyochapishwa leo (24 March 2015). “Ninajua watoto wangu hawatasema “mama yetu alifariki kwa saratani ya kizazi” Alinukuliwa Angelina Jolie.
Upasuaji alioufanya Angelina Jolie ni kwa ajili ya kumkinga na uwezekano wa kupata saratani ya kizazi ikiwa ni sawa na upasuaji wa kuondoa matiti alioufanya mwaka 2013 lengo ikiwa ni kumuepusha na saratani ya matiti.
Msanii huyo aligundulika kuwa na vinasaba hatari vinavyojulikana kama BRCA1 ambavyo vinamuweka kwenye hatari ya kupata saratani ya matiti na mfuko wa uzazi, wanawake watatu katika familia yao wamefariki kutokana na saratani (cancer).
Upasuaji wa kuondoa kizazi pamoja na mirija ya uzazi unamuondolea Angelina Jolie uwezekano wa kupata watoto. Mwaka 2013 Angelina Jolie alipotangaza kufanyiwa upasuaji wa kuondoa matiti idadi ya wanawake waliojitoketa kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti iliongezeka mara mbili zaidi.