Chama cha Demokrasia na Maendeleo leo Jumamosi 13/02/2016 katika ofisi za Jimbo la Ubungo kimewashukuru wananchi wa Ubungo na Kibamba kwa pamoja kwa kuchagua Ukawa kwa kura nyingi za udiwani pamoja na wabunge, na kupelekea CCM kuwa Chama cha Upinzani kwenye Majimbi haya kuanzia wenyeviti wa S/Mtaa/Udiwani mpaka Wabunge na jiji kwa ujumla.
Akiongea mbele ya waandishi wa habari Katibu Uenezi Jimbo la Ubungo Bw. Perfect John Mwasiwelwa amesema “Kama chama na viongozi wa Chama jimbo la Ubungo ikiwa na majimbo mawili, tumeamua kuchukua hatua hii kuzungumza nanyi waandishi ili Watanzania na Wananchama wetu kutambua kuwa kama Chama tumeamua kuchukua hatua na kutoa neno letu kwa Watanzania juu ya sintofahamu iliyogubikwa katika uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar es salaam”.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanalinda Umoja wa Katiba wa Wananchi UKAWA na kuamua kujitokeza na kukemea na kupinga upotevu wa haki za kimsingi kabisa kwa Watanzania wa Dar es salaam kwa kukosa kuwa na kiongozi wao wa kisiasa katika mkoa wa Dar es salaam, lakini kubwa ni kutoa rai kwa vyombo husika kuacha haki itendeke na kuitaka Serikali na vyombo vyake kutoingilia mchakato huu wa kumpata Meya wa jiji la Dar es salaam. Kuhusu Hali Ya Kisiasa Visiwani Zanzibar.
Suala la Zanzibar Bw. Mwasiwelwa amesema “Tunaitaka Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kutopuuza msimamo wa Chama Cha Wananchi CUF na msimamo wa Wazanzibar juu ya mustakabali wa nchi yao ya Zanzibar hatuwezi kukaa na kuongelea mustakabali wa nchi pasipo kupata muafaka wa Zanzibar wito wetuni kuitaka serikali kuacha mara moja kuwanyima Wazanzibar haki yao ya Kikatiba na kutaka aliyeshinda apewe haki yake”.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamekitaka Chama cha Mapinduzi kuacha kutaka kuipoteza amani ya Zanzibar, CHADEMA chama ambacho kimsingi mbali ya kuwa ndiyo chama kikuu cha upinzani nchini lakini ndiyo chama kinachoongoza na kusimamaia Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, wamemtaka Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mhe. Paul Makonda kutoingilia shughuli za kiutendaji za baraza la madiwani kitendo kinachopelekea kuchonganisha baraza la madiwani na wananchi.
Bw. Perfect Mwasiwelwa amemtaka DC Makonda aache mara moja kuwanyanyasa wananchi wa Manispaa ya Kinondoni haswa wafanyabiashara wadogo wadogo pembezoni mwa barabara kwa kuwa kama Manispaa imeshaandaa utaratibu mzuri wa kuwafanya wafanyabishara wafanye biashara zao kwa ustaarabu na kulinda mazingira, “Anachokifanya DC Makonda tunasema ni unyanyasaji na akiendelea tutamchukilia hatua za kisheria” aliongeza Katibu Uenezi Jimbo la Ubungo Bw. Perfect Mwasiwelwa.
Siku 100 za Rais Magufuli. Siku 100 za Rais Magufuli kama Msemaji wa Chama Jimbo la Ubungo, Bw. Mwasiwelwa akiongelea suala hilo amesema “Rais Magufuli ameshindwa kwa sababu alitoa ahadi lukuki wakati wa kampeni ikiwa ni kurudisha na kufufua viwanda vyote vya UMMA na vilivyo na ubia na Serikali lakini la pili ni kutoa Elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne” Kikubwa sio Elimu bure Rais Magufuli anatakiwa afanye maboresho ya kimsingi katika sekta hiyo muhimu kwa taifa, vile vile aliahidi kurejesha mashamba makubwa yanayokodiwa na watu wachache kwa manufaa yao.
Amesema Rais Magufuli ameshindwa japo ni mapema kumuhukumu kwa siku chache lakini muelekeo na mwenendo wa serikali yake unaonyesha wazi kuelekea kushindwa kutokana na kukurupuka kwa watendaji wake na kufanya kazi kwa misingi ya kazi husika.
Pia Katibu Uenezi Jimbo la Ubungo Bw. Perfect John Mwasiwelwa alimpongeza Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Boniface Jacob kwa kuanza vizuri utendaji wake kwa Manispaa ya Kinondoni na kufanikiwa kupata wafadhili kujenga kiwanda cha kutenegeneza mbolea itokanayo na taka taka.