DAKTARI wa Hospitali ya Temeke, jijini Dar es Salaam, Dk. Gilbert Bubelwa, amefariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuugua ugonjwa wa homa ya Dengue. Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho jana kwa njia ya simu, Msemaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Algaeshi, alisema daktari huyo ambaye alilazwa hospitalini hapo tangu Alhamisi ya wiki iliyopita, alifariki dunia juzi, saa saba usiku.
“Ni kweli dokta huyo amefariki dunia jana (juzi) usiku majira ya saa saba baada ya kuzidiwa, lakini pia kwa hospitali hii (Muhimbili) ni wagonjwa watatu wengine walipokelewa, wawili wanafunzi na mmoja ni staff, hali zao zinaendelea vizuri,”alisema Aligaeshi.
Msemaji wa Hospitali ya Temeke, Joyce Msumba, akizungumza kwa njia ya simu, alisema kuwa kwa sasa wamebakiwa na wagonjwa watatu ambao ni wauguzi wawili na daktari mmoja.
Alisema hadi sasa bado hajawafahamu majina yao huku akisisitiza juhudi za makusudi zinafanyika kuwanusuru na ugonjwa huo.
Alisema ugonjwa wa Dengue kwa Wilaya ya Temeke hasa katika hospitali hiyo unatokana na mazingira yao na kwamba wanaendelea kumwaga dawa, ili kuua mbu wanaoeneza ugonjwa huo.
“Ugonjwa huu unatokea hapa hapa kutokana na mazingira, na kwamba juhudi za makusudi zinafanyika, tayari ‘fumigation’ inafanyika kuua mbu na pia tunahamisha wagonjwa kutoka wodi moja kwenda nyingine ili tuweze kupuliza dawa kwa umakini,” alisema Msumba.
Alieleza wakati ugonjwa huo unatokea, wauguzi na madaktari katika hospitali hiyo waliacha kwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kutoa huduma wakihofia kupatwa na maradhi hayo.
Ugonjwa wa Dengue umeingia jijini Dar es Salaam kwa kasi ambapo baadhi ya watu kadhaa wameripotiwa kuugua ugonjwa huo, wakiwemo wasanii Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’, Rehema Chalamila ‘Ray C’, Mbunge Bahati Ally Abeid (CCM) ambaye naye ameripotiwa kulazwa katika hospitali ya Dk. Mvungi iliyopo Kinondoni Dar es Salaam.
Ugonjwa huo unaoenezwa na mbu aina ya Aedes, umesambaa mkoani Dar es Salaam na kuathiri wilaya zote tatu za Temeke, Ilala na Kinondoni.