Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda yupo chini ya ulinzi huku akitibiwa majeraha katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Sheikh Ponda alisafirishwa usiku wa manane kutoka Morogoro baada ya juzi kupigwa na kitu kinachodaiwa kuwa ni mtutu wa bomu saa 12:25 jioni alipokuwa akisindikizwa na wafuasi wake kwenda katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja mara baada ya kumaliza kutoa mhadhara katika kongamano mjini hapo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kongamano hilo, Sheikh Idd Mussa Msema, alidai kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi tatu begani.
Taarifa kutoka ndani ya familia ya Ponda zilisema kwamba baada ya kupata taarifa za kupigwa risasi, baadhi ya masheikh walifunga safari kwenda Morogoro na kumrejesha Dar es Salaam usiku huohuo.Kabla ya kurudishwa Dar es Salaam, imeelezwa kuwa Sheikh Ponda alipelekwa katika Zahanati ya Islamic Foundation.
Mmoja wa wanafamilia alidokeza kwamba Sheikh Ponda alifichwa na alikuwa chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wake na hakuna aliyeruhusiwa kumsogelea.
Muhimbili
Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye jana zilisema kuwa alifikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Sheikh Ponda alifikishwa Muhimbili jana saa 7:18 mchana na alipelekwa kwenye chumba cha wagonjwa wa dharura na baadaye alitolewa na kupelekwa kwenye chumba cha x-ray kwa ajili ya vipimo. Baadaye alipelekwa chumba cha upasuaji.
Eneo kubwa la hospitali hiyo lilikuwa na idadi kubwa ya askari na mmoja wa askari waliokuwa doria hospitalini hapo alisema walitawanywa kwenye hospitali mbalimbali za Dar es Salaam baada ya kupata taarifa kuwa angeletwa kwa matibabu.
“Nakuambia tuko hapa tangu saa kumi na moja asubuhi, tumetawanywa hospitali mbalimbali baada ya kupata taarifa kuwa analetwa Dar. Bahati nzuri kaletwa hapa Muhimbili… tunasubiri apate matibabu na tutamtia mbaroni,” alisema askari huyo.
Taarifa ya polisi
Msemaji wa Polisi, Advera Senso alisema jana katika taarifa yake kuwa Sheikh Ponda yuko Hospitali ya Muhimbili akitibiwa baada ya kupata majeraha yaliyotokana na purukushani na polisi wakati wafuasi wake walipokuwa wanataka kumtorosha.
“Kutokana na tukio hilo, timu inayoshirikisha wajumbe kutoka Jukwaa la Haki Jinai likiongozwa na Kamishna wa Polisi Isaya Mungulu imeanza uchunguzi wa tukio hilo na Polisi inawataka wananchi kuwa watulivu wakati wanashughulikia suala hilo kisheria.”
Polisi Morogoro wapigwa chenga
Wakati akiwa Muhimbili, Polisi mkoani Morogoro, lilisema bado linamtafuta Sheikh Ponda.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile alisema jana kuwa kwa taarifa zilizopo, bado Sheikh Ponda amefichwa mkoani Morogoro na kwamba anaendelea kutafutwa.
“Tamko la Serikali mpaka sasa hatujathibitisha kwamba Sheikh Ponda amejeruhiwa na risasi na tunamtaka mtu yeyote awe yeye au ndugu yake aje kuthibitisha kwamba amepigwa risasi,” alisema.
Alikanusha madai kwamba jeshi hilo limehusika kumpiga risasi akisema hakuna ushahidi kwa kuwa hajaonekana ili kuonyesha kuwa amepata majeraha sehemu yoyote ya mwili wake.
“Siku zote risasi haifichiki, kama amepigwa angejitokeza ili kupewa kibali cha matibabu,” alisema Shilogile.
Alisema polisi inawashikilia watu wawili na inawatafuta viongozi watano wa Umoja wa Waadhiri wa Kiislamu Mkoa wa Morogoro walioandaa kongamano hilo.
Kamanda Shilogile alisema waandaaji wa kongamano hilo walipewa kibali na polisi kufanya kongamano kwa masharti ya kutokutoa matamshi ya uchochezi ikiwa ni pamoja na Sheikh Ponda kutokuhudhuria.
Alisema hata hivyo, katika kongamano hilo lililofanyika eneo la Kiwanja cha Ndege kulikuwapo na wageni zaidi ya watano waliohutubia.Kamanda Shilogile alisema ilipofika saa 12.50 jioni ndipo Sheikh Ponda alipofika na baadaye kupewa dakika tano kuzungumza na alieleza kuwa yeye si mzungumzaji kwa siku hiyo na badala yake angezungumza leo katika Viwanja vya Msikiti wa Jabal Hirra.
Alisema baada ya hapo mkutano ulifungwa na wafuasi wake wakaanza kusukuma gari alilokuwa amepanda katika Barabara ya Tumbaku karibu na Kituo cha Mafuta cha El Saedy.Alisema kuwa, polisi walimfuata kutaka kumtia mbaroni lakini wafuasi wake walianza kurusha mawe na ndipo askari hao walipofyatua juu risasi tatu za baridi ili kuwatawanya.
Hata hivyo, alisema polisi walizidiwa nguvu na wafuasi hao ambao walifanikiwa kumtorosha Sheikh huyo kwa pikipiki.Alisema kuwa baadaye zilizagaa taarifa kuwa amepigwa risasi ya begani na kupelekwa Hospitali ya Mkoa kisha kutoroshwa kusikojulikana.
Wavamia hospitali
Katika hatua nyingine, watu wanaosadikiwa ni wafuasi wa Sheikh Ponda wamevamia Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kufanya uharibifu kwa kuvunja vioo katika wodi namba sita ya watoto wakishinikiza kuonyeshwa Sheikh huyo alipo.
Baadhi ya wagonjwa waliolazwa na watoto wao katika wodi hiyo, Kibua Michael na Cecilia Clemence kwa nyakati tofauti walisema kwamba wafuasi hao walikusanyana nje ya hospitali hiyo na kurusha mawe na kusababisha taharuki kwa baadhi ya wagonjwa.
Sheikh Kundecha atoa sharti
Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, imeitaka Serikali kuunda tume huru ya uchunguzi wa tukio la kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda na majibu yake ndiyo yatakayoamua uhusiano baina ya Waislamu nchini na Serikali iliyopo madarakani.
Akitoa tamko la Jumuiya hiyo katika Msikiti wa Mtambani, Kinondoni, Dar es Salaam jana, Amiri wa Jumuiya hiyo, Sheikh Yusufu Mussa Kundecha alisema pamoja na mambo mengine, pia wanataka kuona askari polisi aliyemdhuru Sheikh Ponda anachukuliwa hatua za kisheria.
Alisema kitendo alichofanyiwa Sheikh Ponda ni mtiririko wa vitendo vya uonevu na unyanyasaji na aliishangaa Serikali kumtafuta Sheikh huyo kupitia vyombo vya habari wakati inafahamu hatua za kuchukua pale wanapokuwa wanamtafuta mtu.
Alisema hata yeye wakati anatafutwa na polisi alipelekewa barua akitakiwa kuripoti kituoni lakini si kupitia vyombo vya habari na kitendo hicho kinaonyesha wazi kuwa Serikali imeshindwa kuwahakikishia raia usalama wao.
“Mbaya zaidi, wao ambao wanataka watu wasichukue sheria mkononi ndiyo hao wa kwanza kufanya hivyo jambo ambalo sidhani kama litatufikisha pazuri,” alisema Kundecha.
Aliitaka Serikali kufuata sheria na kufuata taratibu husika katika kushughulikia masuala yanayowahusu makundi mbalimbali katika jamii badala ya inavyofanya sasa akisema hiyo inachangia chuki kati ya Waislamu na Serikali.
Profesa Lipumba atoa tamko
Mwenyekiti wa (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati suala la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda ili nchi isije kuingia kwenye machafuko yenye mrengo wa kidini.
Profesa Lipumba aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake Dar es Salaam kuwa chama hicho kinalaani vikali tukio hilo na kutaka polisi kuwakamata waliompiga risasi.
“Nimetoka kumjulia hali muda mfupi uliopita, nimemkuta akiwa katika hali mbaya japo anaweza kuzungumza na kutambua watu wanaokwenda kumwona… kwa kweli tukio la kupigwa risasi kwa Sheikh Ponda linaweza kusababisha nchi kuingia kwenye machafuko ya kidini kama hatua za haraka hazitachukuliwa.
“Tukio la Sheikh Ponda kupigwa risasi tena na watu wanaodhaniwa kuwa ni polisi, limeleta sura mbaya kwa taifa,” alisema Lipumba.
Rufaa ya wafuasi wake leo
Wakati hayo yakitokea, rufaa ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda waliohukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela inatarajiwa kusikilizwa leo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Wafuasi hao walihukumiwa kifungo hicho, Machi 21, mwaka huu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu kati ya manne yaliyokuwa yakiwakabili.
Walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama, kutenda makosa, kukaidi amri ya polisi kabla na baada ya kufanya maandamano yaliyozuiwa na polisi, kufanya mikusanyiko haramu na kusababisha uvunjifu wa amani na uchochezi.
Hata hivyo, kupitia kwa Wakili wao, Mohamed Tibanyendera walikata rufaa wakipinga hukumu na adhabu waliyopewa.
Rufaa hiyo itasikilizwa leo na Jaji Salvatory Bongole.
Kwa mujibu wa hati ya rufani waliyoiwasilisha mahakamani hapo, wafuasi hao, pamoja na mambo mengine, wanadai kuwa hakimu alikosea kisheria katika kuchambua ushahidi wa pande zote uliowasilishwa mahakamani.
Pia wanadai kuwa katika hukumu hiyo, hakimu alijikanganya kwa kumwachia huru mmoja wa washtakiwa na kuwatia hatiani washtakiwa wengine.
Watu hao walikamatwa na Polisi Machi 15, mwaka huu, wakiandamana kwenda Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa lengo la kumshinikiza kumpa dhamana Sheikh Ponda na mshtakiwa mwenzake Mukadam Swalehe na Machi 18, mwaka huu walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka.-Mwananchi