
Na hii ndio nyumba Ya Mama Yake Iliyopo Karibu Na Nyumba Za Mwanae
Akitangaza ratiba ya kuwasili kwa mwili na maziko ya Waziri Mgimwa kwa waandishi wa habari jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema shughuli zote zitafanywa na serikali.
Lukuvi alisema tayari serikali imeshaunda kamati mbili, moja ipo jijini Dar es Salaam, ina wajumbe kutoka Ikulu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo itaongozwa na yeye.
Alisema kamati ya pili imeundwa mkoani Iringa ambayo itashughulikia namna ya kuuhifadhi mwili wa marehemu Mgimwa kijijini kwake Magunga, ambayo itaongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Christine Ishengoma.
Lukuvi alisema mwili wa Mgimwa utawasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini, majira ya saa saba mchana katika Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (Terminal II) na kupelekwa nyumbani kwake Mikocheni B, na itakapofika majira ya saa 11 jioni utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo alisema siku ya Jumapili, mwili wa Mgimwa utawasili nyumbani kwake majira ya saa 5:30, kisha utapelekwa katika Ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya ibada, heshima za mwisho na salamu za rambirambi hadi saa nane mchana.
Alisema mara baada ya tukio hilo, mwili wa Mgimwa utapelekwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (Teminal I) kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Iringa ambapo unatarajiwa kufika majira ya saa 10 jioni ili kuwapa fursa wananchi wa mkoa huo kuuaga katika Ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Lukuvi alisema mara baada ya wananchi wa Iringa mjini kuaga, jioni hiyo hiyo mwili wa Mgimwa utapelekwa kijijini kwake Magunga kwa ajili ya kupumzishwa kesho yake (Jumatatu).
“Shughuli za kuwasili na hatimaye maziko zinafanywa na serikali kupitia kamati kuu na ile ya Mkoa wa Iringa, ambayo itapata mwongozo kutoka huko chini ya Dk. Ishengoma,” alisisitiza Lukuvi.
Mgimwa alifariki dunia juzi nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa kwa matibabu.
Kijijini Mgimwa
