Matukio ya Watoto kutekwa na Watu wasiojulikana katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam na viunga vyake, yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara na kusababisha baadhi ya Familia Jijini humo kukumbwa na hofu kubwa ya Watoto wao kutekwa. Taarifa za kuwepo
kwa matukio hayo zilizozuka kwa kasi hapa Jijini zinalilazimu Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam kutolea ufafanuzi kwa kubainisha kuwa taarifa hizo za Watoto kutekwa hazina ukweli wowote. Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, CP SULEIMAN KOVA anaeleza kushangazwa na uvumi huo na kuwataka Wakazi wa jiji hilo kutokuwa na hofu yoyote ya Watoto wao kutekwa na kuhakikisha wanawapeleka Watoto wao shule kama kawaida. Katika hatua nyingine Kamishina KOVA amesema idadi ya Watu waliopoteza maisha kutokana na kulipukiwa na lori la mafuta lililopinduka eneo la Mbagala zakiem Jijini Dar es salaam imeongezeka na kufikia watano. Mbali na tukio hilo Kamishina KOVA amesema Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata Jambazi anaedaiwa kuhusika na kifo cha Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Usalama wa Taifa nchini, Silvanus Mzeru, katika mataa ya barabara iliyoko karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu JULIUS NYERERE.