Kufuatia kuandamwa na skendo za wanaume na kuchafuliwa kila siku, mama mzazi wa staa wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael Kimemeta ‘Lulu’, Lucresia Karugila ‘Mama Lulu’ ametoa kauli nzito yenye kushtua kwamba anatamani mwanaye huyo afe tu ili watu wanyamaze kumsemasema. Imemuuma sana!
Mama Lulu amefunguka hayo siku kadhaa baada ya mitandao ya kijamii kuchafuka kwa habari za binti yake na wanaume hasa wa watu huku mwenyewe (Lulu) akiwa nyumbani kwake Mbezi-Beach jijini Dar akiwa hana hili wala lile.
Akizungumza na gazeti la Risasi, mama Lulu alisema mambo mazito kuwa, hakuna mzazi ambaye hata siku moja anaweza kuvumilia kuona mtoto wake akiandamwa na kashfa ambazo si za kweli.
“Mimi ndiye nimemzaa Lulu, najua uchungu wa mtoto kama mzazi.
“Wanaomsema Lulu vibaya wakumbuke hata mimi nina moyo kama wao, si chuma hivyo hata mimi naumia kama ambavyo mwanamke yeyote mwenye kujua uchungu wa mwana ni nini anaweza kuumia.“Ni mzazi gani mwenye moyo wa chuma wa kuona mwanaye anabebeshwa shutuma nzito kama hizo kila kukicha halafu akanyamaza au kufurahia?
“Watu wanamfuatilia na kumsakama sana mwanangu. Hawamwachi apumue,” alisema mama Lulu kwa uchungu huku machozi yakimtoka.
Chanzo:GPL