Katika kipindi cha mwezi April 2016, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya shilingi Trilioni 1.035 ambayo ni sawa na asilimia 99.5 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.040 katika mwezi huo.
Makusanyo ya kipindi cha miezi kumi (Juali 2015 hadi Aprili 2016) ni jumla ya Shilingi Trilioni 10.92 sawa na asilimia 99 ya lengo la shilingi Trilioni 11.02 katika lengo ya kipindi hicho.
Kwa kipindi cha miezi miwili iliyobaki TRA imedhamilia kukusanya zaidi ya shilingi trilioni 1.4 ili kufikia na kuvuka lengo la mwaka 2015/2016 ambalo ni shilingi trilioni 12.3
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo kuhusu mwenendo wa makusanyo ya mapato, Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Alphayo Kidata amesema TRA inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha inafikia na kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali inazokabiliana nazo.
“Kwa kipindi hiki cha miezi miwili iliyobaki, TRA imejiwekea mikakati thabiti ya kuongeza mapato ili kuweza kufikia au kuvuka lengo kwa mwaka huu wa fedha ikiwemo; kuendelea kupambana na magendo, kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kusimamia mifumo ambayo inamrahisishia mlipakodi kulipa kodi anayostahili bila usumbufu wowote” alisema Kamishna Mkuu
Bw. Kidata amesema TRA inaendelea kudhibiti wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine za kielektroniki za kodi (EFDs) kwa kuwakamata na kuwatoza faini au kuwafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Hadi sasa wafanyabiashara zaidi ya 300 nchi nzima wamekamatwa na kutozwa faini ya shilingi 746,400,000/= kwa makosa ya kutotoa risiti, kutoa risiti yenye bei pungufu na kutotumia mashine za kielektroniki. Baadhi ya wafanyabiashara miongoni mwa waliokamatwa walihukumiwa kifungo au kulipa faini.
Wafanyabiashara hao wakipatikana tena na makosa hayohayo watapelekwa mahakamani nam kuhukumiwa kifungo kisicho pungua miaka mitatu jela kwa kukahidi agizo la serikali.
“TRA haitowavumilia wafanyabiashara wanaoikosesha mapato serikali kwa kuuza na kutoa huduma bila risiti za EFDs kwa makusudi, wafanyabiashara wanaouza kazi wasanii bila stempu za kodi, pamoja na wafanyabiashara wanaojihusisha na magendo.”
“Tumeshaanza kuwapeleka mahakamani wafanyabiashara ambao wanakwepa kulipa kodi kwa kuuza bidhaa bila risiti, pia tumetaifisha bidhaa mbalimbali zilizoingizwa nchini kwa njia za magendo hasa kwa zile bidhaa ambazo zitathibitika kuwa salama kwa matumizi ya binadamu zitatolewa kwa watu au taasisi zenye uhitaji” Alisema Kamishna Mkuu
Mamlaka inatoa wito kwa wananchi kuwa mabalozi wa kodi na kichocheo cha ukusanyaji wa mapato kwa kudai risiti za EFDs pale wanaponunua bidhaa ama kupatiwa huduma, kutoa taarifa kwa Mamlaka kuhusu wale wote wanaojihusisha na biashara za magendo, wafanyabiashara wanaouza kazi za wasanii ambazo hazijabandikwa stika ya kodi na ukwepaji kodi wa namna yoyote ile.
“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”
Imetolewa na:
Idara ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi
TRA- Makao makuu