Takriban watu watano wameuawa katika shambulizi lengine katika eneo la pwani ya Kenya.
Mauaji hayo yametokea karibu na eneo ambako mashambulizi mengine yalifanyika wiki jana na kusababisha vifo vya watu zaidi ya sitini.
Maafisa wanasema kuwa kundi la watu waliokuwa wamejihami walivamia kijiji cha Watu ambacho kiko umbali wa kilomita 15 kutoka mji wa Mpeketoni.
Hakuna aliyedai kufanya mashambulizi hayo hadi kufikia sasa.
Kundi la wapiganaji wa kiisilamu nchini Somalia, al-Shabab lilikiri kufanya mashambulizi ya wiki jana katika mji wa Mpeketoni karibu na Lamu.
Rais Uhuru Kenyatta, hata hivyo aliwalaumu wanasiasa kwa mauaji hayo.
Mkuu wa jimbo la Lamu, Stephen Ikua, alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo usiku wa kuamkia leo.
Al-Shabab, lilisema kuwa mashambulizi ya hapo awali yalikuwa ya kulipiza kisasi kwa kuwepo wanjeshi wa Kenya nchini Somalia.
Ndege za kivita za Kenya zilifanya mashambulizi mengine dhidi ya kambi za wapiganaji wa Al Shabaab na kuwaua wapiganaji 80 mwishoni mwa wiki.