Makao makuu ya kanisa Katoliki duniani Vatican, yametangaza kuwa mchakato wa uchaguzi wa papa mpya utaanza tarehe 12 Machi mwaka huu.
Chini ya sheria za mchakato huo, ambao unafanyika kwa njia ya kura ya siri, makardinali 115 wa kikatoliki watachagua hadi mgombea atakapopata theluthi mbili ya kura zote.
Kitengo cha habari cha Vatican kimesema kutafanyika ibada ya misa Jumanne asubuhi kabla ya kuanza kwa zoezi la kupiga kura mchana wa siku hiyo.
Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Benedict wa 16, alijiuzulu mwezi Februari baada ya karibu miaka nane ya uongozi wa kanisa hilo.Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 85 ndiye papa wa kwanza kujiuzulu katika kipindi cha miaka karibu 600.