
Kikundi cha Mbwa Mwitu ambacho awali kilisambaratishwa na Jeshi la Polisi kiliibuka tena Mei 19 mwaka huu katika eneo la Kigogo safari hii kikijipachika jina la Panya Road na kuanza kufanya uhalifu katika maeneo ya Jangwani, Ilala, Karume na kuleta hofu miongoni mwa jamii.
Jeshi la Polisi Kanda Maalum kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hatimaye likadhibiti hali hiyo kwa kuwakamata vijana 175 kwa kuendesha vitendo vya kiuhalifu ikiwemo kupora madukani, barabarani na majumbani.
Licha ya kukamatwa kwa vijana hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam SAID MECKY SADICK amezungumza na Watendaji wa Manispaa ya Kinondoni ikiwemo Maafisa Watendaji, Wenyeviti wa Mitaa ili kuwahamasisha kuwafichua wazazi wanaoficha watoto wao wahalifu.
Mkuu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishina SULEIMAN KOVA ambaye anaongoza kampeni hiyo, anatumia fursa hiyo kutangaza kuanza kwa msako wa nyumba kwa nyumba ili kuwakamata vijana wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu Jijini humo.
