
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa hakuna ugonjwa wa Ebola nchini Nigeria, ikiwa ni baada ya kupita siku 42 bila kushuhudiwa kesi mpya ya maambukizo ya ugonjwa huo. Rui Gama Vaz mwakilishi wa WHO amesema leo akiwa katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja kwamba, hivi sasa hakuna ugonjwa wa Ebola nchini Nigeria na kwamba hii ni habari ya kuvutia ya mafanikio inayoudhihirishia ulimwengu kuwa ugonjwa
wa Ebola unaweza kuangamizwa. Nigeria imekuwa nchi ya pili magharibi mwa Afrika kutangazwa kuwa imeangamiza ugonjwa wa Ebola, baada ya WHO kutangaza wiki iliyopita kuwa Senegal pia haina tena ugonjwa huo. Nchi hiyo yenye idadi kubwa ya watu barani Afrika, ilipokea sifa tele kwa hatua zake za kukabiliana haraka na virusi vya Ebola baada ya mwanadiplomasia Mliberia mwenye ugonjwa huo kwenda Nigeria mwezi Julai. Inaelezwa kuwa wananchi wa Nigeria waliipa umuhimu hatari ya ugonjwa huo na kuzingatia ipaswavyo maelekezo ya maafisa wa afya ya kukabiliana na ugonjwa huo.
