
OMBAOMBA mmoja nchini Marekani, ameshinda kitita cha dola 50,000 (takriban sh. milioni 82) katika bahati nasibu, amekataa kununua nyumba badala yake ataendelea kuishi mitaani.
Jamaa huyo aliyefahamika kama Dennis Mahurin (58), amekuwa akiishi mitaani akiombaomba tangu mwaka 1978, na hajawahi kuwaza kufanya shughuli yoyoye ya kumuingizia kipato.
Mahurin alinunua tiketi ya dola 3 katika kituo kimoja cha mafuta na kuikwangua, ambapo alibahatika kujishindia kitita hicho kisha kuipeleka sehemu husika kujinyakulia zawadi hiyo.
Hata hivyo, awali alidhani alikuwa ameshinda dola 1,000 takriban sh. milioni 2 kabla ya ofisa wa bahati nasibu kumueleza kwamba alishinda kitita cha dola elfu 50 ambacho ni cha juu zaidi.
“Nilikwangua tiketi hapa hapa kwenye kibanda changu hiki nikijua kuwa nimeshinda dola 1,000 kisha nikaipeleka kituo cha bahati nasibu, lakini nilielezwa kuwa nilishinda dola 50,000,” anasema Mahurin.
Akizungumzia zaidi alisema hawezi kubadili maisha yake kwa vile hiyo ndiyo asili yake na anafurahia maisha aliyo nayo pamoja na kuwa ameshinda kitita kikubwa cha fedha.
Pamoja na yote hayo, amepanga kuwatembelea ndugu zake na kuhifadhi fedha alizopata na kueleza kuwa atawagawia dola 100 kila mmoja ili nao waishi maisha mazuri.
Aidha, ombaomba huyo anasema kuwa kiasi kingine cha fedha atawagawia wenzake anaoshinda nao mitaani wakiomba chochote kutoka kwa wapita njia.
