
Rais Jakaya Kikwete amepongeza ushirikiano ulioonyeshwa na wadau wote walioshiriki kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kunasua miili ya watu waliofukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 kuanguka jijini Dar es salaam machi 16 mwaka huu, ambapo watu 34 walipoteza maisha.
Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza na kuwashukuru wadau hao iliyofanyika katika ukumbi wa PTA jijini Dar es salaam, Rais Kikwete amesema ushirikiano huo ni kitendo cha upendo na huruma, kinachopaswa kuigwa kwa kuwa kimerahisisha utendaji kazi katika suala zima la uokoaji.
Ametumia fursa hiyo kuzitaka mamlaka husika ikiwemo Kamati ya Maafa ya mkoa wa Dar es salaam kuendeleza jitihada ilizokwishachukua kuhakikisha waliosababisha jengo hilo la ghorofa 16 kuporomoka na kusababisha vifo, wanachukuliwa hatua za kisheria.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Said Meck Sadick, akitoa taarifa ya mkoa amesema ofisi yake imedhamiria kutomuacha yeyote ambaye kwa namna moja ama nyingine amehusika katika kusababisha maafa
Katika hafla hiyo Rais Kikwete amekabidhi vyeti vya utambuzi kwa makundi maalum yalishiriki kikamilifu kutoa huduma za hali na mali kufanikisha zoezi hilo ambapo
waliokabidhiwa ni Kamati ya Maafa, Timu ya wataalamu wa uokoaji wa mkoa, Vikosi vya zimamoto na uokoaji, mitambo , vikosi vya uokoaji na watoa huduma, Huduma na matibabu, Ulinzi na usalama, Huduma za mahitaji ya jamii na baadhi ya vyombo vya Habari, ambapo Mhariri wa habari wa Channel ten Esther Zelamula, amepokea cheti kwa niaba ya Kampuni ya Africa Media Group inayomiliki vituo vya Channel Ten, DTV, CTN na Redio Magic FM.
Hafla hiyo ilianza kwa sala na dua kutoka kwa viongozi wa dini.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam jumla ya maheruhi 18 walitibiwa kufuatia maafa ya kuporomoka kwa jengo hilo na mpaka sasa majeruhi 16 wamesharuhusiwa , wawili bado wamelazwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.
————————————
