Sakata la kusambazwa kwa picha chafu kwenye mitandao mbalimbali limeibuka tena Bungeni Mjini Dodoma baada ya Mbunge wa Mkanyageni HABIBU MOHAMED MNYAA kuhoji kitendo cha Serikali kushindwa kudhibiti vitendo hivyo.
Katika swali lake la nyongeza MNYAA amesema licha ya Serikali kuipatia Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA mitambo ya kubaini chanzo cha picha chafu kusambaa imeshindwa kufanya hivyo, hali inayochangia kuharibika kwa maadili ya Watanzania.
Akijibu swali hilo Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa MAKAME MNYAA MBARAWA amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wamekuwa wakiwachukulia hatua wahusika kila yanapojitokeza malalamiko.
Majibu hayo ni kama hayamfurahishi Spika ANNE MAKINDA ambaye anaamua kuingilia kati kutaka kupata ufafanuzi juu ya hatua zilizochukuliwa baada ya picha chafu za Wabunge JOHN KOMBA na SALVATORY MACHEMLI kusambazwa mitandaoni.
Sakata hilo lililoibuliwa na Mbunge wa Mchinga SAID MTANDA nusura liingie katika hatua nyingine baada ya Mbunge JOHN KOMBA kusimama kutaka kuchangia hoja, hata hivyo kiti cha Spika kikaingilia kati na kulizima suala hilo.
Bunge liliahirishwa hadi leo saa tatu asubuhi kupisha kamati ya Bajeti kupitia baadhi ya marekebisho tayari kwa Bajeti kuu kusomwa Juni 12 mwaka huu.