Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba SAMWEL SITTA amewataka watu wanaomchukia wasihusishe chuki zao na Bunge la Katiba analoliongoza kwani mchakato wa
Katiba ni suala la Kitaifa.
Akizungumza bungeni mjini Dodoma baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji FREDRICK WEREMA kutolea ufafanuzi maamuzi yaliyotolewa na mahakama kuu ya Tanzania kuhusu bunge la Katiba, kufuatia kesi iliyofunguliwa na SAID KUBENEA, Mwenyekiti wa Bunge amesema hatishiki na vitisho vyovyote vinavyotolewa dhidi yake.
Katika ufafanuzi wake Jaji WEREMA amewataka wajumbe wa Bunge la Katiba kutulia na kufanya kazi yao mpaka pale watakapotoa Katiba inayopendekezwa.
Baada ya utangulizi huo ikaja fursa ya Kamati za Bunge kuwasilisha maboresho ya Ibara mbalimbali za rasimu ya Katiba inayopendekezwa, ambapo mwakilishi wa Kamati namba Tano PAUL MAKONDA amesema ipo haja ya kuongezwa kwa Ibara mpya itakayoainisha kuanzishwa kwa chombo cha kuisimamia mahakama, ili iweze kutenda haki kwa wananchi pindi inapocheleweshwa.
Uwasilishwaji huo wa taarifa za Kamati za Bunge unatoa fursa kwa Kamati ya Uandishi inayoongozwa na ANDREW CHENGE kufanya marekebisho katika Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, iliyowasilishwa bungeni mapema wiki hii, ili kutoa Katiba itakayopigiwa Kura na wabunge kuanzia Septemba 29 mwaka huu.