
Waziri Mkuu wa Ukraine Arseniy Yatsenyuk amesema Uholanzi inapaswa kuongoza uchunguzi wa kubaini aliyeilipua ndege ya shirika la ndege la Malaysia MH17, amesema Kiev iko tayari kusafirisha miili yote nchini Uholanzi.
Waziri Mkuu Yatsenyuk wa Ukraine amesema Uholanzi, nchi ilioathirika pakubwa kwa kuwapoteaza raia wake wengi katika ajali ya MH17 inapaswa kuongoza Uchunguzi, na kwamba wako tayari kukabidhi uratibishaji kwa wenzao wa Magharibi.
“Nasema tena kwamba tuko tayari kutoa ushirikiano juu ya uratibu wa uchunguzi kwa uholanzi, nchi ambayo imeathirika pakubwa katika mkasa huu, na kuishirikisha jamii yote ya Kimataifa.” Alisema Yatsenyuk.
Akizungumza na vyombo vya habari mjini Kiev, Yatsenyuk amesema bado Ukraine inaamini ndege hiyo ya abiria ilidunguliwa na wataalamu walio na uwezo wa kutumia kombora la BUK-M1.
Amesema hii inaonesha wazi kuwa makombora ya aina hii hayawezi kutumiwa na waasi wanaoiunga mkono Urusi, huku akiishutumu moja kwa moja Urusi kwa kuiangusha ndege hiyo.
Waziri Mkuu huyo wa Ukraine amesema rais wa Urusi Vladimir Putin anapaswa kuelewa yale aliyoyafanya hadi sasa yanatosha, akimshutumu kwa kutoa silaha kwa waasi wanaopambana na utawala wa Ukraine Mashariki mwa nchi hiyo.
