Wanasayansi wanaamini kuwa wamepata sababu moja mpya ya kwa nini tunahitaji usingizi.
Wanasema kuwa kulala kunasaidia katika kujenga celi mpya za ubongo
Usingizi unasaidia kuzalisha upya celi za ubongo ambazo nazo hujenga kemikali inayojulikana kama Myelin ambayo ni muhimu katika kulinda ubongo wetu kwa ambavyo unafanya kazi.
Matokeo ya utafiti huu ambayo yalijitokeza katika panya wa mahabara, huenda yakachochea maelezo zaidi kuhusu umuhimu wa usingizi katika kukabarabati celi za ubongo na kukuza celi mpya pamoja na kuulinda kutokana na magonjwa.
Daktari Chiara Cirelli na wenzake kutoka chuo kikuu cha Wisconsin waligundua kuwa Panya hao walipokuwa wanalala, ndipo kemilaki hiyo ilikuwa inatengezwa kwa wingi na celi za mwili.
Ongezeko la kemikali pia ilitegemea aina ya usingizi ambao Panya walilala hasa uliohusishwa na ndoto.
Kinyume na hilo, celi zilionekana kufariki wakati Panya walipokuwa wako macho wazi.
Na hii ndio maana usingizi ni muhimu jambo ambalo wamekuwa wakilihoji wanasayansi kwa miaka mingi. Yaani nini umuhimu wa usingizi?
Ni wazi kuwa tunahitaji kulala ili kupumzika na ili ubongo wetu ufanye kazi vyema….lakini mambo ya kibayolojia yanayofanyika tunapokuwa tumelala ndio yameanza tu kugunduliwa.
Daktari Cirelli alisema kuwa : “kwa muda mrefu, watafiti wa usingizi wamekuwa wakilenga tofauti iliyopo kati ya celi za neva wakati wanyama wanakuwa hawajalala na wakti wamelala. Kwa sasa ni bayana kuwa celi zengine kwenye mfumo wa neva hubadilika kutokana na usingizi.”
Watafiti hao wanasema kuwa matokeo yao yanapendekeza kuwa ukosefu wa usingizi,unaweza kusababisha maradhi ya ubongo yanayoathiri celi zake.
Watafiti hao pia wanataka kuchunguza ikiwa vijana kukosa usingizi wakati wanapokuwa huenda ikaathiri ubongo wao katika siku za usoni.
Usingizi ni muhimu kwa mfumo wa neva mwilini ili uweze kufanya kazi vyema.
Usingizi pia husaidia katika uzalishaji wa homoni zinazowafanya watoto na vijana kukuwa.
Chanzo: BBC