Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa mwito wa kuyasimamisha mapigano mara moja wakati ambapo majeshi ya Israel yanaendelea na mashambulio katika Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa taarifa mpaka sasa Wapalestina zaidi ya 500 wameshauawa. Askari 18 wa Israel pia wameuawa katika vita vinavyoendelea ndani ya Ukanda wa Gaza
Wakati jumuiya ya kimataifa inaziimarisha juhudi ili mapigano yasimamishwe katika Ukanda wa Gaza,Israel imesema asakari wake wamewaua wapiganaji 10 wa Hamas katika mapambano ya bunduki yaliyotokea mapema asubuhi leo. Kwa mujibu wa Israel wapiganaji hao wa Hamas walijaribu kujipenyeza ndani ya Israel kwa kupitia katika njia ya chini ya ardhi kwenye mpaka.
Rais Barack Obama pia ameurudia mwito juu ya kuyasimamisha mapigano mara moja katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mapema leo, wakati ambapo Waziri wake wa mambo ya nchi za nje John Kerry akiwapo Mashariki ya Kati katika juhudi za kuyasimamisha mapigano.
Lakini Israel imeendelea na mashambulio leo. Watu tisa kutoka ukoo mmoja wameuawa kutokana na shambulio la ndege katika mji wa kusini wa Rafah. Saba kati ya waliouawa walikuwa watoto. Shambulio hilo lilitokea baada ya Wapalestina zaidi ya 150 kuuawa, hapo jana , yaani siku mbaya kabisa kwa Wapalestina tokea Israel ianze mashambulio siku 14 zilizopita.
Kwa upande wake Israel imesema askari wake 13 waliauwa jana pekee ,ndani ya Ukanda wa Gaza na hivyo kuifanya idadi ya Waisraeli waliouawa tokea majeshi ya Israel yaingine katika Ukanda wa Gaza ifikie 18 .
Idadi ya Wapalestina waliouawa hadi leo Jumatatu ni zaidi ya 500 ukiwaondoa wapiganaji 10 waliojipenyeza ndani ya kusini mwa Israel.Askari wa Israel walipambana na Wapalesttina hao na kuwaua .Lakini askari kadhaa wa Israel pia walijeruhiwa.
Mjumbe wa Shirika la misaada la Umoja wa Mataifa aliepo ugani kwenye Ukanda wa Gaza Robert Turner pia metoa mwito wa kuyasimamisha mapambano mara moja