Waziri Mkuu MIZENGO PINDA ameagiza kufanywa kwa ukaguzi wa kina kwa magari yote yanayoingizwa nchini kutoka nje, ili magari yenye Ubora yaweze kuingia kwa ajili ya matumizi ya Serikali na watu binafsi, kwa lengo la kupunguza ajali za barabarani ambazo husababisha vifo na majeruhi.
Akijibu swali la mbunge wa Kilwa MURTAZA MANGUNGU, aliyetaka kuwekwa kwa utaratibu maalum wa ukaguzi wa magari yanayoingizwa nchini, katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu MIZENGO PINDA amesema kuingizwa kwa magari mabovu, licha ya kuchangia ongezeko la ajali pia yamekuwa yakichangia uwepo wa msongamano hasa katika majiji makubwa.
Katika hatua nyingine Bunge limeridhia azimio la kukifanya chuo cha Maendeleo Tengeru kilichopo mkoani Arusha, kuwa Taasisi inayojitegemea ili kukiwezesha kuzalisha wataalamu wa kutosha wa maendeleo ya Jamii, watakaofanya kazi Serikalini na katika Sekta binafsi ili kuleta maendeleo.
Wakichangia hoja hiyo kwa nyakati tofauti, baadhi ya wabunge akiwemo wa Iringa mjini Mchungaji PETER MSIGWA, na mbunge wa Viti Maalum ESTHER BULAYA, wameshauri serikali kutotelekeza chuo hicho baada ya kuwa Taasisi, na badala yake Serikali ielekeze nguvu zake katika kuiboresha ili kutatua changamoto zilizopo, ikiwemo ubovu wa miundombinu na kujenga uwezo wa kufungua matawi kwenye mikoa mingine.
Awali akiwasilisha bungeni Azimio hilo, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi JENISTER MHAGAMA amesema, wameamua kukipandisha hadhi chuo hicho ili kukiwezesha kuhimili ushindani katika soko la ajira, na kuongeza idadi ya watalaamu watakaokuwa wakitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali ya kimaendeleo kwenye jamii.
Kwa upande wao Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii MARGARET SITTA, na msemaji wa Kambi rasmi ya Upinzani bungeni RAJAB MBAROUK, wameshauri kutatuliwa kwa migogoro ya ardhi kwenye chuo hicho, na kukipatia Hati Miliki sanjari na kuendelea kukitengea fedha.