SHIRIKISHO la Filamu Tanzania (TAFF) limempongeza msanii wa kike Wema Sepetu kwa moyo wa upendo aliouonyesha kwa msanii mwenzie Kajala Masanja kwa kumlipia faini ya sh. milioni 13 alizotozwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na kupatikana na hatia katika kesi ya utakatishaji fedha iliyokuwa inamkabili mahakamani hapo.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wengine rais wa shirikisho hilo Simon Mwakifwamba alisema kuwa imani na moyo wa upendo aliokuwa nao msanii Wema ndio uliomsukuma kumlipia kiwango hicho cha fedha bila ya kujiuliza mara mbili kitendo hiko kimeonyesha jinsi gani wanavyohitaji kushirikiana katika matatizo.
Alisema kuwa wasanii wanatakiwa kujifunza kutoka kwake kwani wanahitaji kuwa kitu kimoja kujaliana kwenye matatizo na kutambua kuwa wao ni familia moja wanaojenga nyumba moja
“Kitendo alichoonyesha msanii mwenzetu ni kitendo cha kuigwa na cha kiimani siyo kwamba anauwezo sana hapana ila kujali na utu ndio kilichomsukuma atoe fedha hizo” alisema Mwakifwamba”