Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni linamshikilia Ahmad Mohamed Sharif (38), mfanyabiashara na mkazi wa Mwananyamala Msisiri ’A’ kwa tuhuma za kuwaingilia kinyume cha maumbile wanafunzi wanne wa darasa la nne wa Shule ya Msingi Misisiri ’A’. Ahmad amekuwa akiwaingilia kinyume cha maumbile wanafunzi hao katika kipindi cha mwezi Aprili na Mei mwaka huu kwa nyakati tofauti. Kati ya wanafunzi hao, wawili wana umri wa miaka 10 na wengine wawili wana umri wa miaka 12 na 11 wote wakiwa ni wanafunzi wa Misisiri A.Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Suzana Orege (35) alisema wanafunzi hao wamekuwa na mahudhurio mabaya shuleni kwa zaidi ya mwezi mmoja na ndipo walipojaribu kuwafuatilia kwa karibu ili kubaini sababu za wanafunzi hao kutohudhuria shuleni. Suzan alisema ilipofika Mei 9, mwaka huu walifanikiwa kuwapata wanafunzi watatu (majina yanahifadhiwa) lakini mmoja alikimbia kusikojulikana na walipowahoji sababu za wao kutohudhuria masomo, waliwaeleza kuwa huwa wanatoka nyumbani kama kawaida kwa ajili ya kwenda shule, lakini huishia nyumbani kwa Ahmed. Alisema walipohojiwa zaidi walisema baada ya kufika nyumbani kwake huwawekea CD za ngono na kisha kuwaingilia kinyume cha maumbile na kuwapa maandazi, chapati, bagia, biskuti na kuwatishia wasiseme kwa mtu yeyote na endapo watasema atawafanyia kitu kibaya . Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Kenyela amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, ambapo alisema alikamatwa Mei 10, mwaka huu na atafikishwa mahakamani kesho. Kamanda ametoa onyo kwa watu wengine wenye tabia chafu kama hiyo kuacha mara moja kabla ya kukumbwa na mkono wa sheria.