
Arjen Robben ameomba msamaha baada ya kujirusha katika mechi ambayo Uholanzi ilishinda 2 – 1 katika mzunguko wa 16 wa mwisho lakini amesema haikuwa kwa lengo baya ili apate penati.
Kocha wa Mexico Miguel Herrera amemshutumu Robben kwa kujirusha mara tatu katika mchezo ule lakini mchezaji huyo wa Uholanzi kupitia televisheni ya nchi hiyo aliomba radhi.
Robben amesema lakini ile ya mwisho ilikuwa ni penati kweli baada ya kuchezewa faulu na mchezaji wa Mexico Rafael Marquez katika dakika ya 94 lakini Herrera alisema mchezaji huyo hata hakutakiwa awepo uwanjani na asingeweza kupata penati, Herrera alisema kwamba Robben aliruka mara tatu.
Mexico walikuwa na woga wa penati kuelekea mwishoni mwa kipindi cha kwanza wakati Robben alipodondokea eneo la hatari baada ya kukabwa na Hector Moreno.
Refa wa Kireno Pedro Proenca alipeta na Mexico wakafunga goli na kuongoza mapema katika kipindi cha pili pale Giovani Dios Santos alipofunga akiwa umbali mrefu.
Ikiwa ni muda wa nyongeza katika kipindi cha pili, Robben aliingia katika eneo la Mexico ndipo Marquez alipocheza kiatu kwa Robben na kumfanya refa atoe penati ambayo vizuri ilifungwa na Huntelaar na kuifanya Uholanzi kufuzu.
Penati hiyo imemfanya kocha wa Mexico Herrera kusema kwanini FIFA walichagua refa kutoka katika shirikisho hilo hilo kama Uholanzi badala ya refa kutoka Amrika kusini, Asia au Afrika?
