Siku ya Jumapili ya tarehe 26 mwezi huu, uzinduzi wa shindano la Big Brother Africa utaonyeshwa moja kwa moja katika luninga ambapo utapambwa na burudani kabambe itakayoporomoshwa na wanamuziki waliowahi kushinda tuzo kadhaa kutoka Nigeria, Kenya na Afrika Kusini.
Katika usiku huo wa uzinduzi nchi zaidi ya 50 za Afrika zitashuhudia kutambulishwa kwa washiriki wapya 28 watakaoingia katika mjengo wa Big Brother ‘season 8’ uliobatizwa jina la Big Brother ‘The Chase’.
Shoo hiyo hiyo itaonyeshwa ‘live’ katika luninga kupitia AfricaMagic, AfricaMagic Entertainment, AfricaMagic World sambamba na DStv channel 197 na 198.
Mashabiki watapata fursa ya kusikiliza muziki murua kutoka Kenya kutoka kwa msanii aliyewahi kushinda tuzo kadhaa zikiwemo Kisima Awards, Clops Awards na Jeermaan Awards ambaye pia ni muimbaji, muandikaji wa nyimbo na rapa STL anayetamba na nyimbo za “Take My Time” , “Hula Hoop”, na “Bad as I Wanna Be”, aliyehidi kushusha burudani ya uhakika katika ladha tofauti za Pop, Soul na Rap Sound.
Wakitua kutoka Nigeria, wakali wa muziki mzito Don Jazzy, D’ Prince na Wande Coal pia watakuwepo kuwashika mashabiki wa uzinduzi huo kwa nyimbo zao maarufu kama vile “I like What I See”,“Bumper 2 Bumper” na“Who Born the Maga”.
Funga kazi ni moja kundi tishio la muziki wa Afro pop kutoka Afrika Kusini “Mafikizolo” linalotarajiwa kuangusha mawe mazito yakiwemo ”Sibongile”, “NdihambaNawe”, “Nisixoshelani” na kibao chao kipya cha “Khona”.
Kama vile haitoshi uzinduzi wa Big Brother Africa ‘The Chase’ utapambwa na shoo ya mchekeshaji maarufu wa Kenya Daniel Ndambuki maarufu kama ‘Churchill.
Shoo ya Big brother Africa itakuwa pia ikionyeshwa katika mtandao wa www.bigbrotherafrica.com, ambapo unachochotakiwa kufanya ni kuwa na kompyuta iliyounganishwa na intanet.
Baada ya uzinduzi mfululizo wa shindano lenyewe la Big Brother Africa ‘The Chase’ utakuwa ukionyeshwa ‘live’ kwa saa 24 kwa siku saba kwa kipindi cha siku 91 katika DStv kupitia Channel 91 na 198 wakati watazamaji wa GOtv watakuwa wakiona vidokezo katika Africa Magic World.