
(Inatolewa chini ya Kanuni ya 99(9) ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2013)
1. UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Dira ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ni “kuwa na taifa lililohabarishwa vizuri, lina vijana wenye uwezo na malezi bora, linathamini utamaduni wake na linakuwa mahiri katika michezo ifikapo mwaka 2025.” Aidha, ‘dhamira’ ya wizara hii ni ‘kuendeleza utambulisho wa taifa kwa kuwezesha upatikanaji mzuri wa habari, kuwawezesha vijana kiuchumi na kukuza utamaduni na michezo kwa umma kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.’
Mheshimiwa Spika,
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Serikali hii ya CCM imeshindwa kutekeleza dira na dhamira iliyotajwa katika maandiko ya kisera ya Wizara. Badala yake, chini ya usimamizi wa Wizara hii, Tanzania imegeuka kuwa taifa lisilotaka watu kuhabarishwa vizuri juu ya matendo ya watawala.
2. UHURU WA UHARIRI NA USALAMA WA WANAHABARI
Mheshimiwa Spika,
Kwa masikitiko makubwa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalitaarifu Bunge lako tukufu kwamba sasa Tanzania imeingia rasmi katika orodha ya fedheha (The List of Shame) ya mataifa ambayo taaluma ya habari ni taaluma ya hatari kwa wale wote wanaoitumia kama sehemu ya wajibu wao kwa taifa na kama ajira yao.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa ya CPJ, tishio kubwa kwa waandishi wa habari duniani ni kuuwawa kwa kutekwa na kuteswa na/au kutishiwa maisha. Aidha, Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ni washiriki wakubwa wa mauaji ya waandishi wa habari.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya CPJ inaungwa mkono na ushahidi wa matukio mengi yanayodhihirisha kwamba maisha ya waandishi wa habari wa Tanzania yako hatarini kutokana na vitendo na vitisho kutoka kwa Serikali na watendaji wake ambao hawataki kusikia ukweli dhidi yao ukianikwa hadharani. Kudhihirisha kauli hii tunaomba kumnukuu mwanahabari mahiri na mmoja wa wahanga wa vita dhidi ya wanahabari na uhuru wa habari hapa nchini, Mzee Ndimara Tegambwage:
“Mwaka 2006, waliojiita wananchi wakazi wa jiji la Mwanza, walikusanywa na wenye uwezo kufanya maandamano makubwa kwa walichoita ‘kupinga mwandishi Richard Mgamba kuandika uongo’ na kudai kwamba alikuwa Mkenya na ‘siyo raia wa Tanzania.’ Desemba 2009, mwandishi Frederick Katulanda wa Mwanza, alivamiwa nyumbani. Wavamizi walikuwa wakipaza sauti na kudai kuwa ana nyaraka za akaunti za benki za Halmashauri ya Jiji la Mwanza. Walikuwa na mapanga. Walikuwa wakichagizana kwa kusema, “Kata kichwa! Kata kichwa!” Waliondoka na mafaili. Walimwachia kilema mguuni na makovu mikononi.
“Mwezi Septemba, 2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, katika eneo la Nyambiti, Jimbo la Sumve wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, mwandishi Frederick Katulanda alivamiwa na kupigwa na watu wapatao 15 waliojiita “Green Guard” – wa “chama cha kijani.” Katika “kumshughulikia,” Katulanda anasema, walikuwa wakionyesha kuwa na ujuzi mkubwa wa judo na karate huku wakidai kuwa anawaandika ‘vibaya’ Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mwaka 2011 mwandishi Richard Massatu alikutwa amekufa katika eneo la Igoma, jijini Mwanza. Vyombo vya habari viliripoti kuwa macho yake yalikuwa yametobolewa na kuwekwa gundi aina ya super glue; mguu wa kushoto na mbavu vilikuwa vimevunjika. Vyombo vya habari viliripoti kuwa Massatu aliyekuwa mmiliki na mhariri mkuu wa gazeti la Kasi Mpya (sauti ya umma), alionekana mara ya mwisho usiku wa kifo chake akiwa na maofisa wa polisi na usalama katika baa iitwayo Cross Park katika eneo la Igoma.
“Tarehe 3 Januari, maiti ya mwandishi Issa Ngumba iliokotwa katika pori la mlima Kajuruheta, kijiji cha Mhange, wilayani Kakonko katika mkoa wa Kigoma.Ngumba alikuwa mwandishi wa habari wa Redio Kwizela. Tangu mwezi uliopita Machi, mwandishi wa habari Erick Kabendera anayeishi Dar es Salaam, anaishi kwa wasiwasi. Wazazi wake waishio Bukoba, wamehojiwa na ‘ofisa usalama’ kwa kile kilichoitwa ‘uhalali wa uraia wao.’
“Kuuwawa kwa aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Luninga cha ITV, John Lubungo ambaye alikuwa mfuatiliaji mahiri wa habari zinazohusu wafanyabiashara au biashara haramu ya dawa za kulevya ambayo inadaiwa kufanywa na watu wakubwa nchini, wakiwemo vigogo serikalini.
Kwa sababu ya uadilifu na kutopenda kujikweza, Mzee Tegambwage hakutaja shambulio la tindikali na mapanga dhidi yake na mwandishi mwenzake Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi, ambalo baadae lilifungiwa na Serikali hii ya CCM.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria ya tarehe 3 Mei mwaka huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilielezea kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali hii ya CCM imekuwa tishio kwa maisha ya waandishi wa habari na kwa uhuru wa habari katika nchi yetu.
Kwa mujibu wa Ripoti ya MCT/TEF, matokeo ya uchunguzi wao “… yanadhihirisha bila wasi wasi kwamba polisi kwa makusudi waliwavurumisha waandishi waliotoka Iringa wakati wakikusanya habari za shughuli za CHADEMA katika kijiji cha Nyololo.
Hata amri ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Mafinga Mwampamba kuwataka askari polisi waache kumpiga marehemu Mwangosi haikusikilizwa na askari hao. Ili kujiokoa, marehemu Mwangosi alimkumbatia OCS Mwampamba na “baadaye kumwangukia miguuni mwake kuepuka kipigo zaidi.”
Mheshimiwa Spika,
Sio MCT/TEF pekee zilizofanya uchunguzi wa mauaji ya Marehemu Mwangosi. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nayo ilitoa Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Uchunguzi wa Tukio Lililopelekea Kifo cha Daudi Mwangosi Kilichotokea Septemba 2, 2012 Kijijini Nyololo, iliyobaini kwamba Marehemu Mwangosi “… alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye … alipigwa bomu na kufa papo hapo.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa hiyo, “…
Mheshimiwa Spika,
