
Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya nchini Kenya imeagiza kuchunguzwa kwa fomu 34 za matokeo ya uchaguzi wa rais kutoka katika vituo vyote 34,400, vilivyotumika kupigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo uliofanyika Machi 4, mwaka huu.
Kadhalika mahakama hiyo jana iliagiza kuhesabiwa upya kwa kura za urais katika vituo vya kupigia kura 22 kati ya elfu 33 vilivyolalamikiwa na aliyekuwa mgombea urais wa Muungano wa Cord, Raila Odinga.Katika malalamiko yake yaliyowasilishwa katika mahakama hiyo kupinga Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa urais katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Machi 4, Odinga alidai kuwa vituo hivyo 22 kura zilizopigwa zinazidi idadi ya wapigakura walioandikishwa.Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya majaji wenzake watano, Jaji Smokin Wanjala alisema kwamba uhesabuji kura wa vituo hivyo utafanyika leo kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa lengo la kubaini ukweli kuhusu madai hayo.
