MSHTUKO mkubwa ulijiri Jumamosi iliyopita, ikiwa ni baada ya kusambaa kwa habari za kumwagiwa tindikali, mfanyabiashara mwenye ‘levo’ ya ubilionea, Said Said Mohammed, 42, ambaye ndiye mmiliki na Mkurugenzi Mkuu wa Home Shopping Centre. Said ambaye kwa utambulisho mwingine anajulikana kama Said Mohammed Saad, alimwagiwa tindikali Ijumaa iliyopita, saa 2 usiku, lakini habari zake zikavuma Jumamosi, hivyo kuibua taharuki ya aina yake.Kuhusu nani alimmwagia tindikali hiyo, sababu ya kutendwa unyama huo, yupi mhusika mkuu wa ukatili wenyewe na malengo ya uharamia, kwa jumla, hayo ni maswali yanayoendelea kuitesa familia yake, watu wa karibu pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania.
Taarifa za kipolisi zinathibitisha kwamba alimwagiwa tindikali akiwa anazungumza na mfanyakazi wake wa duka lake lililopo kwenye Jengo la Msasani City Mall kisha akakimbizwa Hospitali ya Ami Wellness Centre, iliyopo Masaki, Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Afrika Kusini kwa ndege ya kukodi ndani ya kipindi kisichozidi dakika 60.SAID NI NANI?Ni Mtanzania mwenye asili ya Bara la Asia. Inadaiwa kwamba ndugu zake wengi wana asili ya nchi za Yemen na Saudi Arabia.Ndiye mmiliki wa Kampuni ya Home Shopping Center.
Kampuni hiyo ina maduka mengi Dar es Salaam na katika mikoa kadhaa ambayo yanahusika zaidi na uuzaji wa vitu vya nyumbani na ofisini.
Anatajwa kuwa tajiri mwenye uwezo zaidi katika jumuiya ya wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo, kifedha na ushawishi.
Inadaiwa kwamba wafanyabiashara wengi wenye maduka yao Kariakoo, humtegemea yeye kuingiza mizigo nchini, kutokea nje ya nchi hususan China.
Anamiliki nyumba kadhaa za ghorofa Kariakoo, yapo madai kwamba anamiliki nyumba sita.Baadhi ya majengo ambayo anahusishwa nayo, la kwanza lina ghorofa saba, lipo Mitaa ya Swahili na Msimbazi, la pili lina ghorofa sita, lipo Kongo na Aggrey, tatu ni la ghorofa nne, lipo Barabara ya Uhuru na kadhalika.
Said kupitia kampuni yake ya Home Shopping Centre, aligeuka nyota ya jaha kwa familia 655, zilizokumbwa na mafuriko eneo la Jangwani, Desemba 2011 kisha kuhamishia Mabwepande, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa moyo wake mwema, Said aliidhinisha kila familia ipewe seti kamili ya vyombo vya nyumbani pamoja na taa zinazowaka kwa kutumia nishati ya mwanga wa jua.Misaada hiyo, ilikabidhiwa na mkurugenzi mwingine wa Home Shopping Centre, Ghalib Said Mohammed ambaye ni mdogo wa Said.
Misaada hiyo, ilipokelewa na Rais Jakaya Kikwete, Januari mwaka jana.Said hakuishia hapo, baada ya misaada ya vyombo na taa za nishati ya mwanga wa jua, alifanya jambo jema zaidi kwa kujenga shule ya msingi, madarasa yote pamoja na ofisi za walimu, vilivyojengwa kwa ufadhili wa Home Shopping Centre.
Machi mwaka huu, shule hiyo ilizinduliwa na Rais Kikwete ambaye alikiri kwamba ujenzi wake utarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwenye eneo hilo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Dar es Salaam, Yusuf Mrefu, alisema kuwa uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio la Said kumwagiwa tindikali Julai 19, mwaka huu.
Mrefu alisema, Said alikuwa akizungumza na mfanyakazi wake nje ya duka lake kwenye Jengo la Msasani Mall kisha akatokea kijana mrefu mwembamba ambaye alimmwagia kimiminika kinachosadikiwa kuwa ni tindikali.
Kamanda huyo wa polisi aliongeza kwamba mfanyakazi huyo wa Said, Hassan Ahmad, naye alijeruhiwa kidogo katika purukushani hiyo lakini alipopelekwa Hospitali ya Ami Wellness Centre, alitibiwa na kuruhusiwa.
Inadaiwa kuwa Hassan, alipata majeraha baada ya kuanguka, wakati akimfukuza jamaa huyo ambaye alimmwagia tindikali Said.Mmoja wa wauguzi katika Hospitali ya Ami Wellness, alimwambia mwandishi wetu kwamba baada ya Said kufikishwa pale, ilichukua kama nusu saa, akachukuliwa kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, tayari kwa safari ya kwenda Afrika Kusini.
“Hali yake ilikuwa mbaya, lile jicho moja limeathirika sana, kwa kweli sijui kama litaweza kuona tena.
Ila moja litakuwa salama, ukizingatia amepelekwa katika hospitali yenye ubora zaidi. Yule mfanyakazi wake aliumia kidogo tu, alitibiwa na kuruhusiwa siku ileile,” alisema muuguzi huyo.
Kuhusu jina la hospitali aliyopelekwa, alisema: “Hakukuwa na utaratibu wa kuandika rufaa, alichukuliwa tu kupelekwa Afrika Kusini na sasa naamini anaendelea na matibabu vizuri Ila inasikitisha sana, naamini wahusika walitaka kumfanya awe kipofu.” Kwa mujibu wa taswira ya tukio lenyewe, kitendo alichofanyiwa ni umafia na mambo kadhaa yanafaa kumulikwa kwa undani. Mambo hayo ni;Said ana uadui na nani? Aliyemmwagia alijuaje kama yupo pale? Kwa nini tindikali machoni? Ni wazi Said anao maadui ndiyo maana kitu kile kimetendeka.
Bila shaka aliyemmwagia aliambiwa na mtu, huyo anafaa kupatikana.
Bila kupindisha ukweli ni kwamba mmwagaji alikusudia kumfanya Said awe kipofu.
Polisi wanatakiwa kuchunguza nyendo za Said, kuona ana uhasama na akina nani katika biashara au hata kwenye mambo ya kijamii.
Kadhalika, ichunguze mawasiliano ya watu wa karibu na Said, atajulikana mtoa taarifa, hivyo kumpata mhusika wa ukatili pamoja sababu ya unyama wenyewe.
SKENDO ZA SAID Said ameshawahi kuripotiwa na vyombo vya habari katika kashfa mbalimbali, gazeti moja liliwahi kuandika matoleo kadhaa, likimtaja kama mfanyabiashara hatari kwa nchi ya Tanzania. Vilevile, alishawahi kuripotiwa kumfanyia unyama, kijana mmoja raia wa Lebanon ambaye alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na dada yake.
STORY NA MPEKUZI HURU