Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imetangaza kuahirisha zoezi la kuandikisha wapiga kura, lililopangwa kuanza February 15 mwaka huu nchi nzima, na badala yake litaanzia mkoani Njombe pekee February 23.
Katika mkutano baina ya Tume na viongozi wakuu wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa NEC Jaji DAMIAN LUBUVA amesema, zoezi hilo sasa litafanyika katika mkoa huo mmoja wakati vifaa vingine vikisubiriwa.
LUBUVA amesema wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa watafikiwa na zoezi hilo.
Kwa upande wao viongozi wa vyama vya siasa waliohudhuria mkutano huo, akiwemo Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM NAPE NNAUYE, ameitaka Tume kufanya kazi kwa uwazi, huku Mwenyekiti wa Chama cha NCCR MAGEUZI JAMES MBATIA, akibainisha kuwa kukwama kwa zoezi hilo, kunatokana na Serikali kutotilia mkazo utoaji wa fedha.
Ili kuwaondoa wasiwasi viongozi hao, Mwenyekiti wa NEC amesema kazi zote za Tume zinaendeshwa kwa uwazi, na ana imani zoezi la uandikishwaji wapiga kura litakamilika kwa wakati, kutokana na kasi ya utoaji fedha iliyopo Serikalini hivi sasa.