Rais wa Naigeria Goodluck Jonathan amekutana kwa mara ya kwanza na wazazi wa wasichana zaidi ya 200 waliotekwa nyara na kundi la wanamgambo wa Boko Haram, na wasichana waliofanikiwa kukwepa kutekwa na wanamgambo hao.
Akizungumza na waandishi habari baada ya mkutano na wazazi wa wasichana takriban 219 waliotekwa nyara Aprili 15, katika mji wa Chibok, Reuben Abati, msemaji wa serikali amesema rais Jonathan amewahakikishia wazazi kwamba wasichana wanaozuiliwa watarejea nyumbani wakiwa hai.
Abati amesema serikali ya shirikisho la Naigeria imeamua kufanya kila juhudi za kuwaokoa wasichana wanaozuiliwa na kuwajengea maisha mapya wasichana waliobakia mjini Chibok.
“Serikali itawaweka wasichana hawa katika shule nyengine, serikali itajenga upya mji wa Chibok, shule za upili na taasisi nyengine kwa hiyo wasichana hawapaswa kuwa na uwoga wowote,” alisema Abati.
Hata hivyo nyuso za wazazi waliotoka katika mkutano huo hazikuonekana kuwa na matumaini yoyote ya kuwapata wasichana wao hivi karibuni.
Baada ya mkutano huo maafisa wa Usalama waliwazuwiya waandishi habari kuzungumza na wazazi hao.
Katika mkutano huo rais Goodluck Jonathan aliongozana na waziri wake wa Fedha na elimu pamoja na mshauri wake wa usalama wa taifa. Kashim Shettima Gavana wa jimbo la Borno pia alikuwepo katika mkutano huo uliofanyika jana jioni.
Shettima amewahi kumshutumu Jonathan kutofanya juhudi zaidi za kuwaokoa wasichana waliotekwa, pia aliikasirisha serikali kwa matamshi yake kwamba Wanamgambo wa Boko Harram wanasilaha zaidi kuliko jeshi la Naigeria.