Ripoti iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kuhusu ufisadi nchini Afrika Kusini, imemkosoa vikali Rais Jacob Zuma kwa kujinufaisha na pesa zilizotumiwa kuikarabati nyumba yake binafasi katika mkoa wa Kwazulu Natal. Ukarabati huo uligharimu dola milioni 23.
Katika ripoti yake, mdhibiti wa mali ya umma nchini humo,Thuli Madonsela, amesema kuwa Rais Zuma alikiuka sheria za maadili na kujifaidisha na pesa za Umma.
Inaarifiwa Zuma alisisitiza ukarabati huo, ufanywe.
Hata hivyo, ripoti hiyo ilisema kuwa hakudanganya wabunge kuhusu kashfa hiyo. Kadhalika wito umetolewa kuwa Zuma arejeshe sehemu ya pesa hizo ambazo hazikutumika kwa ajili ya usalama wake au vinginevyo.
Vyombo vya habari nchini humo vinadai kuwa baadhi ya pesa za umma zilitumiwa katika kufadhili mahitaji ya kifahari ya bwana Zuma kama bwawa la kuogelea na chumba cha sinema.
Ujio wa ripoti hiyo wakati huu utaathiri sana sifa ya Zuma na chama chake cha ANC, wakati huu ambapo nchi ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu katika kipindi cha wiki sita zijazo.
Chanzo BBC