
Rais Jakaya Kikwete jana aliongoza maelfu ya Watanzania katika maadhimisho ya miaka 49 ya muungano yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na baadaye kusamehe wafungwa 4,180.
Rais Jakaya Kikwete ametoa msamaha kwa wafungwa 4,180 waliokuwa wakitumikia vifungo vyao katika magereza mbalimbali hapa nchini katika kuadhimisha miaka 49 ya muungano.
Wafungwa waliosamehewa ni wanaotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano, ambapo mpaka siku ya msamaha yaani April 26, watakuwa wameshatumikia robo ya vifungo vyao, wafungwa wagonjwa wa Ukimwi, kifua kikuu na kansa ambao wamethibitishwa na jopo la madaktari.
Pia wazee wenye umri wa miaka sabini au zaidi, wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya, wakiwamo walemavu.
Msamaha wa Rais pia umeenda kwa wafungwa walemavu wa mwili na akili na wafungwa ambao hadi siku ya jana walikuwa wameshakaa gerezani kwa muda wa miaka mitano na wameonyesha kuwa na tabia nzuri.
