Wanasiasa wawili wa bunge la Kongres la Chama cha Republican nchini Marekani wamehoji iwapo ziara ya wanamuziki maarufu wa nchi hiyo mume na mke Jay Z na Beyonce nchini Cuba ilikuwa na kibali cha serikali.
Mastaa hao wamepigwa picha kadhaa wakiwa mjini Havana wakisalimiana na mashabiki wao, wakitoka kupata msosi na kutembelea sehemu kadhaa za mji huo wakati wakisherehekea miaka mitano ya ndoa yao.
Hata hivyo vikwazo vya kibiashara vya Marekani vinazuia wamerekani kuitembelea Cuba kwa sababu za kiutalii pekee na anayetaka kusafiri lazima aombe kibali maalum.
Wanasiasa hao Ileana Ros-Lehtinen na Mario Diaz-Balart wametuma barua kwa Idara ya hazina ya Marekani wakiulizia ni aina gani ya kibali walichopewa wanamuziki hao kuitembelea nchi hiyo.
Wamesema vikwazo vya kuitembelea nchi hiyo viliwekwa kwa sababu marekani iliiorodhesha serikali ya Cuba kama taifa linalounga mkono ugaidi na kudai kuwa nchi hiyo ni moja kati ya nchi zenye rekodi mbaya ya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Kwa kawaida sababu za muhimu zinazoweza kumruhusi raia wa Marekani kwenda Cuba ni pamoja na matibabu, kusoma, sababu za kidini, huduma za kijamii na sababi nyingine za kibinadamu.