MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo ameamuru polisi kumkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema pamoja na wanafunzi walioshiriki kurusha mawe baada ya kutokea vurugu zilizotokana na kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa pili, Chuo cha Uhasibu Arusha, Henry Kago (22).
Naibu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Faraji Kasidi jana alitangaza kufunga chuo hicho kwa muda usiojulikana kutokana na vurugu zilizotokea chuoni hapo, ikiwemo ukiukwaji wa nidhamu na urushwaji wa mawe uliofanywa na wanafunzi hao kwa Mkuu wa Mkoa na kamati ya ulinzi na usalama.
Mulongo alitoa amri hiyo baada ya Lema kudaiwa kuingia chuoni hapo jana asubuhi na kufanya siasa bila kufuata utaratibu.
“Si jambo jema kwa Mbunge kuingia chuoni na kuhamasisha siasa kwenye jambo hilo la kifo badala ya kuwatuliza wanafunzi ili tujue kiini cha tatizo hili,” alisema mkuu wa mkoa na kushutumu kwamba jambo hilo linabadilika badala ya msiba linawekwa chuki za siasa na wanafunzi nao kuingia kwenye mkumbo.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, upo utata wa kifo cha Kago kutokana na wengine kudai ameuliwa na bodaboda eneo la Esami na Kanisa la Waadventista Wasabato karibu na chuo huku wengine wakidai alitoka eneo la Bugaluu.
Alisema polisi inachunguza utata wa kifo hicho cha mwanafunzi huyo aliyekutwa na simu yake ya mkononi.
“Naagiza polisi kumkamata Lema popote alipo na wanafunzi wengine pamoja na wakili wake,” alisema Mkuu wa Mkoa bila kutaja jina la wakili.
Kwa mujibu pia wa RADIO FIVE ya jijini Arusha, Mkuu huyo wa mkoa wa Arusha bwana Mulongo amenukuliwa kwa nyakati tofauti tangu jana akitaja uwezekano wa Lema kusababisha kifo cha mwanafunzi ili apate nafasi ya kufanya siasa chuoni hapo.