Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba jana aliliteka Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma, alipowasilisha Rasimu ya Katiba na kushangiliwa katika maeneo mengi nyeti na kupigiwa kelele katika vipengele vichache vya uraia na ardhi.
Katika hotuba yake ya maneno 14,112 iliyosomwa kwa saa 3:34, Jaji Warioba aliweka wazi maoni ya wananchi yaliyomo katika ibara 271 za Rasimu hiyo, ukiwamo muundo wa Muungano wa Serikali Tatu – Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.
Mwanasheria huyo alijenga hoja zake zilizoisaidia Tume yake kufikia hitimisho la muundo huo, kwamba ilizingatia maoni ya wananchi, yakiwamo ya mabaraza ya katiba ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambayo ama moja kwa moja au kwa tafsiri yalipendekeza muundo wa Serikali Tatu.
Alisema tume hiyo ililazimika kupendekeza muundo huo kutokana na kero, hoja na malalamiko yaliyotolewa na pande mbili za Muungano wakati tume hiyo ikukusanya maoni, pamoja na hoja zilizotolewa miaka ya nyuma na tume mbalimbali.
“Suala la muundo wa Serikali Tatu limechukua nafasi kubwa katika mjadala tangu tume ilipozindua Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Mjadala wa muundo wa muungano umekuwa mkubwa kiasi cha kufunika mapendekezo mengine yaliyomo katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano,” alisema Warioba katika hotuba yake ya aya 191 ambayo imechapwa kwa ukamilifu ndani ya gazeti hili.
Huku akishangiliwa na baadhi ya wajumbe, Jaji Warioba alisema kwa tahmini ya tume hiyo, muundo wa Serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa.
“Muungano wa Serikali mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye Serikali mbili na siyo nchi mbili zenye Serikali mbili,” alisema.
Alisema muundo wa Serikali mbili unaweza kubaki tu ikiwa orodha ya mambo ya muungano haitapunguzwa bali itaongezwa na isipokuwa hivyo Serikali ya Muungano itabaki na rasilimali na mambo ya Tanzania Bara tu.
“Katika hali hiyo, pande zote mbili zitaendelea kulalamika. Kwa upande mmoja, Zanzibar itaendelea kulalamika kwamba Tanzania Bara imevaa koti la Muungano kwa faida yake na kwa upande mwingine, Tanzania Bara itaendelea kulalamika kwamba mambo yasiyo ya Muungano ya Tanzania Bara na rasilimali zake, ndizo zimekuwa Muungano,” alisema.
Warioba alishangiliwa tena na baadhi ya wajumbe aliposema: “Muundo wa Serikali Tatu haupunguzi uimara wa Muungano na muungano huo ni wa nchi mbili kwa manufaa ya wananchi, “Faida kubwa iliyopatikana katika miaka hamsini iliyopita ni kuungana kwa wananchi.”
CHANZO: Mwananchi