Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Jihadi limesema mmojawapo wa makamanda wake ameuwawa na shambulio la kifaru karibu na mji ulio kusini mwa Gaza wa Khan Younis.
Hamas imekubali usitishaji wa mapigano wa saa 24 kwa misingi ya kibinaadamu muda mfupi baada ya Israel kutangaza kuanzisha tena mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza baada ya kusitishwa kwa siku nzima ya Jumamosi.
Msemaji wa Hamas Sami Abu Zuhri amesema katika taarifa kwa kujibu ombi la Umoja wa Mataifa la kuingilia kati kwa kufuatilia hali hiyo makundi ya wapiganaji wamekubaliana kwamba usitishaji wa mapigano wa saa 24 uanze kuanzia saa nane mchana.
Zuhri amesema usitishaji huo wa mapigano utazingatiwa kabla ya siku tatu za mapumziko ya Siku Kuu ya Waislamu ya Eid al – Fitr ambayo huadhimisha kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan na inategemewa kuwa Jumanne.
Usitishaji huo wa mapigano kwa misingi ya kibinaadamu umesambaratika huko Ukanda wa Gaza baada ya Israel Jumapili 27.07.2014 kuanza mashambulizi yake mapya kujibu mapigo ya maroketi yaliyovurumishwa kusini mwa Israel na wanamgambo wa Kipalestina.
Vifaru vya Israel na mizinga viliushambulia ukanda huo wa mwambao na kusababisha moshi mzito kufuka angani na kuashiria kumalizika kwa suluhu ya kusitisha mapigano ya saa 24 iliojiamuliwa yenyewe hapo awali.
Taarifa ya jeshi la Israel imesema katika taarifa kufuatia mashambulizi ya maroketi ya Hamas katika muda wote wa suluhu hiyo ambayo imezingatiwa kwa maslahi ya wananachi wa Gaza jeshi hivi sasa linaanzisha mashambulizi yake ya anga, majini na nchi kavu katika Ukanda wa Gaza.
Muda mfupi baada ya hapo mapambano yalizuka kati ya vikosi vya Israel na wanamgambo wa Gaza na sauti za milipuko ya mabomu zimekuwa zikirindima katika eneo zima la Gaza.