Shirika la Save the Children limeitaja Somalia kuwa nchi mbaya zaidi duniani kwa akina mama, na limetoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi kuwalinda kina mama na watoto katika maeneo yanayokabiliwa na migogoro.
Shirika la Save the Children lenye makao yake jijini London Uingereza, linakadiria kuwa wanawake 800 na watoto wadogo 18,000 hufariki kila siku duniani kutokana na sababu ambazo zinaweza kuzuwilika. Ripoti ya shirika hilo yenye kichwa cha habari cha “Hali ya kina mama wa dunia” imesema ni muhimu zaidi kutafuta njia za kukidhi mahitaji ya afya na lishe ya kundi hili lililoko hatarini, katika mataifa yenye migogoro.
Karibu theluthi moja ya vifo vinatokea katika kanda ya Afrika magharibi na Kati, wakati theluthi nyingine inatokea Asia ya Kusini, ambako viwango vya juu vya vifo viko zaidi miongoni mwa makundi ya watu waliotengwa kijamii. Save the Children iliyalinganisha mataifa 178 kwa vigezo vya afya ya uzazi, vifo vya watoto, viwango vya elimu na vipato vya wanawake na hadhi zao kisiasa.
Somalia ilishika nafasi ya mwisho kabisaa, ikiwa chini kidogo tu ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo — ambayo ilishika nafasi ya mwisho mwaka uliyopita — ikifuatia na Niger, Mali na Guinea Bissau.
Mtendaji mkuu wa Save the Children kimataifa Jasmine Whitehead, alisema si jambo la kushangaza kwamba maeneo kumi magumu zaidiya kuishi kina mama ni yale yaliyo na historia ya migogoro ya kutumia silaha, na kubainisha kuwa kina mama walioko katika mataifa maskini ndiyo wanaathirika zaidi.
Miaka mitatu iliyopita Afghanistan ilikuwa mahala pabaya zaidi kwa kuwa mama, lakini sasa nchi hiyo inashika nafasi ya 146 kutokana na hatua ilizozipiga katika kupunguza vifo vya watoto na vile vinavyohusiana na uzazi.
Kwa upande mwingine, Syria imeshuka kutoka nafasi ya 65 mwaka 2011 hadi nafasi ya 115 mwaka huu, baada ya mgogoro kubabisha kuvunjika kwa mfumo mzima wa afya. Ripoti hiyo inasema zaidi ya wanawake milioni 60 walihitaji msaada mwaka huu. Inasema wakati zaidi ya nusu ya vifo vya wazazi na watoto vimetokea katika mataifa yenye migogoro, idadi kubwa ya vifo hivyo ingeweza kuzuwilika.
Finland ndiyo mahala bora zaidi kwa kuwa mama, ikifuatiwa na Norway, Sweden, Iceland na Uholanzi, huku Ujerumani ikishika nafasi ya tisa. Mataifa mengine yaliyomo katika nafasi za juu ambayo si kutoka Umoja wa Ulaya ni pamoja na Australia, Singapore na New Zealand, huku Marekani ikishika nafasi ya 31 na China nafasi ya 61.